TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete leo, Jumanne, Novemba 29, 2011, ametia saini Muswada wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.
Hatua hiyo ya Mheshimiwa Rais kutia saini Muswada huo
inakamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka
2011 baada ya Bunge kuwa limepitisha Muswada huo uliowasilishwa na Serikali
katika kikao kilichopita cha Bunge.
Aidha, kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua
kubwa na muhimu katika safari ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama
ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa
wananchi Desemba 31, mwaka jana, 2010.
Pamoja na kutiwa saini hiyo bado Serikali itaendelea
kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya
kuboresha sheria hiyo.
Hivyo, Mheshimiwa Rais Kikwete anatoa wito kwa mwananchi
yoyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko
huru kutoa maoni yake na Serikali itasilikiza na kuchukua hatua zipasazo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment