Mabaki ya miili 12 iliyoteketea kwa moto katika ajali ya
basi la Deluxe iliyotokea Kibaha mkoani humo wiki hii wakati wa mazishi. (Picha na Yusuph Badi).
SIMU YAMTAMBULISHA!
WAKATI mabaki ya miili ya watu 12 walioteketea kwa moto
katika ajali ya basi la Deluxe yakizikwa jana, mmoja wa abiria waliokufa katika
ajali hiyo, Salome Benjamin (24) alitoa simu yake itumike kutoa taarifa kwa
ndugu zake.
Salome, mwanafunzi wa Chuo cha Mipango Dodoma , ameelezwa kuwa aliwapa mashuhuda hao
simu hiyo na kuwataka wawasiliane na ndugu zake kwamba imeshindikana kwake
kuokolewa hivyo wasihangaike.
Akisimulia jana jinsi mwanawe alivyokufa, baba mdogo wa
Salome, Michael Isamuhyo alisema shuhuda aliyetumia simu ya mwanawe aliwaeleza
kuwa, Salome kabla ya kufa, aliwataka wasihangaike.
Isamuhyo aliyezungumza na gazeti hili, alisema shuhuda huyo
aliwaeleza kuwa Salome kabla ya kufa alitokea dirishani upande wa kulia na
kupiga kelele ya kuomba msaada.
Shuhuda huyo kwa mujibu wa Isamuhyo, alisema walikwenda
kumsaidia lakini walishindwa kwa kuwa alinasa sehemu ya miguu ndani ya basi hilo .
“Shuhuda alituambia kuwa, wakati wanamvuta, walibaini kuwa
hawataweza kumuokoa kwa kuwa sehemu ya miguu ilinasa na alipoona hawezi
kuokolewa, alirusha simu nje kwa shuhuda huyo.
“Baada ya kutoa simu hiyo, alimtaka atueleze sisi ndugu zake
kuwa ameshindikana kuokolewa ili tusihangaike,” alieleza kwa uchungu Isamuhyo.
Baba wa Salome, Benjamin Magige akizungumzia msiba huo
alisema; “Nimempoteza mtoto wangu wa pekee wa kike, nimebaki na mdogo wake wa
kiume tu, walikuwa wawili pekee, nina uchungu sana .
“(Salome) alikuwa amalize chuo keshokutwa tu, ni maumivu
makubwa kwa familia, mama yake kaja lakini hawezi kuzungumza, huu si wakati wa
Serikali kufumbia macho ajali hizi, tuumie wote na tuhakikishe zinakoma,”
alisema Magige huku akilia.
Maiti hao walizikwa katika makaburi yaliyochimbwa kwa
kuambatana katika eneo la Air Msae walipozikwa abiria 25 waliokufa katika ajali
ya basi ya Air Msae mwaka 1999, umbali wa kilometa takribani 10 kutoka
ilipotokea ajali hiyo.
Source: Habari Leo.
No comments:
Post a Comment