Nani kuwalipa Dowans Bilions 111
Je ni nani atalipa Mabilioni hayo, kati ya Serikali na
Tanesco, baada ya Mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali pingamizi
la kutaka kuzuia kusajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania kwa tuzo ya Billion 94 (na
riba ya 7.5% toka Nov 2010) dhidi ya Dowans Tanzania iliyotolewa na Mahakama ya
kimataifa ya usuluishi ya kibiashara ICC?
Wengi tulitarajia hukumu hii, sababu ni nyingi, moja wapo ni
ukweli kuwa Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu walishasema tuzo hii haipingiki,
hivo walienda kupambana wakiwa wameshashindwa (psychologically), hivyo
kilichokuwa kinafanyika ni ucheleweshaji tu.
Mjadala sasa ni nani anastahili kulipa tuzo hii au Mibilioni
hii? kati ya Serikali kupitia wizara ya nishati na madini na Tanesco.
Akitoa maoni yake juu ya hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati
ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe alisema hukumu hiyo ni matokeo ya
siasa mbovu.“Tumeingiza nchi hasara kwa sababu ya uongozi dhaifu na siasa za
makundi ya CCM,” alisema Zitto na kuongeza:
“Hata hivyo, Tanesco hawawezi kulipa fidia hiyo kwani
walilazimishwa kuingia mkataba na hata kuvunja mkataba huo.”
Alisema kamati yake imeshaagiza deni hilo lisitokee katika
hesabu za Tanesco na badala yake lilipwe na Serikali.
“Hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
amegoma kusaini hesabu za Tanesco za mwaka 2010 mpaka Serikali ikubali kubeba
mzigo huo,” alisema Zitto.
Ikiwa hivyo ndivyo, kwamba Tanesco walilazimishwa kuingia
mkataba ule na pia kulazimishwa kuuvunja, je ni nani aliyekuwa akiotoa ushauri
huu wa kisheria, wa kulazimisha kuingia mkataba na baadaye baada ya kuona
mazingira ni mwafaka kwake au kwao kuilazimisha Tanesco kuvunja mkataba?
Je ni mwanasheria mkuu wa serikali, ni waziri wa wizari
husika au ni nguvu fulani juu ya wote hao? Anyway hilo lahitaji mjadala wake,
lakini kwa sasa tuulizane, ni nani alipe deni hili? Kama ni wizara ambayo sote
twajua kuwa bajeti yake ilipita kwa mbinde baada ya kukataliwa mara ya kwanza,
je itakuwa na fungu la kulipa deni hili?
Ikumbuke kwamba tuzo hii ina riba ya asilimia 7.5, hivyo
hakuna hasara yoyote kwa Dowans bali serikali na taifa kwa ujumla, hata hivyo
ni nani mmiliki halali wa Dowans anayestahili kulipwa mabilioni yote hayo? Je
ni huyu Mheshimiwa wetu aliyetajwa mara kadhaa ktk hukumu ya ICC au ni yule
mwarabu aliyekuja na kusema yeye ndio mwenyewe na kuacha maswali mengi kuliko
majibu?
Kama ni yule siwezi kumsemea, hatujui watanzania na wala
hajui matatizo yetu, wala hajui kuwa kuna watu wagonjwa wanakufa kila siku kwa
sababu hospitali hazina dawa na yeye hana pesa ya kununulia wanakufa, au kwamba
kuna shule tena za sekondari hazina madawati wala vitabu vya kiada achilia
mbali maabara na uhaba wa wali, hajui kuwa kuna migomo inayoashiria kuanza ata
kabla muhula wa masomo haujaanza wa vyuo vya elimu ya juu kwa sababu tu ya
wanafunzi wengi wanaostahili kukosa mkopo, siwezi kumsemea, kwa hayajui haya.
Lakini kama ni huyu mheshimiwa wetu, ambaye “tunadhani”
(pengine sivyo) anaijua Bongo yetu kindakindaki, anajuia changamoto zetu zoote,
za elimu, afya, miundombinu, uchumi nk. Huyu naweza kidogo si kumsemea bali
kumuomba awe na huruma kidogo na watanzania “wenzake” (sina hakika), awe na
imani ata kama ni siasa uchwara ndio zimemuondoa katika kiti kile afahamu kuwa
kwa Mungu hakuna kiti kile, hakuna uheshimiwa, hakuna utajiri wala utapewa nafasi
ya mbele kwa sababu ulishinda kesi ICC.
Huyu namuomba avae viatu vya wale kina mama wajawazito
wanaokufa kila siku kwa matatizo ya kukosa huduma bora wakati wa kujifungua, au
ajiweke katika nafasi ya watoto hawa ambao madawati kwao ni msamiati usiokuwepo
kwenye kamusi yao, pengine avae japo kihisia uhusika wa kijana yule aliyeuwawa kwa deni la sh 500 tu!, na labda avae viatu vya ndugu zetu Wazanzibar
na madhira yaliyowakuta hivi karibuni kwa kukosa tu usafiri wa uhakika, roho
nyingi zimepotea.
Mifano ni mingi sana mingine anayo yeye mwenyewe, amewai
pengine kukutana nayo, ya jinsi gani watanzania wana changamoto ambazo
zinahitaji pesa nyingi sana kukabilina nazo na si kutoa katika kile kiduchu
walichobahatika kukipata, pesa haiwezi kutufikisha mbinguni, ata kama
tutajikusanyia pesa na mali nyingi kiasi gani hatuwezi kuondoka nazo,
tutaziacha hapa hapa duniani.
Yawezekana tukasema kuwa twawekeza kwa ajiri ya watoto wetu,
lakini je kwa mali ya dhuruma twaweka msingi gani kwa waridhi wetu? labda salamu za Nabii T. B Joshua za mwaka mpya zinaweza kumpa ujumbe.
Chonde chonde Mheshimiwa kuwa na moyo wa imani kwa watanzania wenzio, samehe tuzo hii au itoe kwa idara au asasi maalumu, labda iboreshe elimu, afya au ata miundombinu, ata kama ni kwa jimbo la Igunga, hii itakupa heshima kubwa mbele ya jamii na dunia kwa ujumla kuliko yale yatakayo tokea iwapo serikali italazimika kukopa ama kuchukua fungu la fedha toka kwenye bajeti ambayo ni finyu kukulipa wewe.
Huu ni mtizamo wangu, binadamu tumeumbwa tofauti, si ajabu wewe au mtu mwingine asikubaliane nao.
Bernard Rwebangira,
Bongo Pix Blog.
No comments:
Post a Comment