HATIMAYE serikali imetangaza rasmi kuwa imeanza kumiliki mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira baada ya kuitaifisha kutoka kwa wamiliki wake.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, katika ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam, wakati alipokutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa lengo la kutoa taarifa ya serikali kwa kamati hiyo jinsi ilivyoshughulikia suala la Kiwira baada ya kuahidi kulifanyia kazi wakati wa mkutano wa 16 wa Bunge mjini Dodoma.
“Kimsingi serikali imeshauchukua mgodi huo na inaumiliki kama tulivyoliahidi Bunge, kuanzia sasa ni mali ya serikali na hakuna mtu mwenye mkono pale,” alisema Waziri Ngeleja.
Alisema baada ya kuuchukua mgodi huo, hatua ambayo inafuata ni kuwalipa wafanyakazi wake ambao walikuwa wakifanya kazi kwa muda mrefu bila kulipwa kutokana na waliokuwa wamiliki kusimamisha uzalishaji.
“Tunawataka wafanyakazi wote wa Kiwira watuelewe kuwa tunaanza kuwalipa kuanzia wiki hii. Kabla ya Novemba mosi, mwaka huu, wanatakiwa wawe wamelipwa fedha zao zote za malimbikizo,” alisema Waziri Ngeleja.
Alisema fedha zitakazolipwa kwa wafanyakazi hao ni mishahara ya miezi 15, ambayo ilikuwa haijalipwa kwa kipindi chote ambacho mgodi huo ulisimama.
Alipotakiwa kueleza kama waliokuwa wamiliki wa mgodi huo, wameshalipwa na wamelipwa kiasi, Waziri Yona alisema hilo litafahamika zaidi mjini Dodoma wakati atakapowasilisha ripoti yake katika mkutano wa 17 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Oktoba 27.
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, William Shellukindo, alisema wamepokea taarifa ya serikali kuhusu mgodi wa Kiwira na wataiwasilisha bungeni.
“Sisi tumewasikiliza serikali na tutakwenda kuwasilisha bungeni, mengi tutakwenda kusema huko,” alisema Shellukindo bila kufafanua zaidi.
Pia alisema kamati hiyo imefurahishwa na uamuzi wa serikali kuumiliki rasmi mgodi wa Kiwira na kuamua kuwalipa wafanyakazi malimbikizo ya mishahara yao ambayo imekuwa ikilalamikiwa kila mara.
Kamati hiyo ilisisitiza kuwa, suala la Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Daniel Yona kulipwa au kutokulipwa na wamelipwa kiasi gani, litajulikana mjini Dodoma.
Hata hivyo, Shellukindo jana aliendelea kugoma kujibu maswali mengi kutoka kwa wanahabari kwa madai kuwa maelezo yaliyotolewa yanatosha.
Azma ya serikali kutaka kurejesha mgodi wa Kiwira mikononi mwake, mara ya kwanza ilitangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa mkutano wa 16 wa Bunge.
Alisema serikali itachukua hisa zote za Kiwira ili kuondoa lawama zinazomkabili kiongozi huyo wa serikali ya awamu ya tatu.
“Mimi nilichoamua... kama issue ya Kiwira ndiyo kitu kikubwa, nitahakikisha zile hisa zote zinarudi serikalini.
“Nitachukua zote, nitazirudisha serikalini tuanze upya ili tuone kuwa hiki tulichoanza nacho, pengine kitatupa tija tunayohitaji,” alisema Waziri Pinda wakati akifanya majumuisho ya hotuba ya bajeti ya ofisi yake.
Inadaiwa kuwa, familia ya Mkapa na Yona, zilitakiwa kununua mgodi huo kwa sh milioni 700, lakini walikubaliwa wakati wa kusaini mkataba walipe Sh milioni 70 na zilizosalia zilipwe katika kipindi cha miezi sita. Hata hivyo, fedha hizo hazikulipwa.
Makampuni mengine ambayo kwa pamoja yaliungana na kununua mgodi huo ni Choice Industries, ambayo wamiliki wake ni Joe Mbuna na Goodyeer Francis na Universal Technologies, ambayo inamilikiwa na Willfred Malekia na Evance Mapundi. Wabia hawa ndio waliounda Kampuni ya Tanpower Resources Ltd inayomiliki mgodi huo.
Mgodi huo umejengwa na Serikali ya China na kukabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania kabla ya kuuzwa kwa wawekezaji wapya Kampuni ya Tanpower, Machi 2007.
source: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment