WATU wawili wamekufa na wengine watatu kunusurika baada ya
lori walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika daraja la Mto Loobuko kati
ya Makuyuni na Mto wa Mbu wilayani Monduli.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 12 alfajiri wakati lori hilo namba T190 AKW likiwa
limebeba mitambo ya kutengeneza barabara likitoka Engaruka kwenda Arusha,
kukumbwa na dhahama hiyo.
Maafa hayo yametokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha
katika milima ya Monduli.
Mfanyakazi wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda
(ICTR), Augustino Masige, akiendesha gari namba T573 AHW, akitoka Arusha kwenda
Musoma ni miongoni mwa watu walionusurika katika maafa hayo baada ya gari lake
aina ya Toyota kusombwa na maji eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga, aliwataja watu
waliokufa kuwa ni dereva wa lori hilo
aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Shekman (38) na msaidizi wa mitambo ya
kutengeza barabara, Samwel Julius (28).
Kasunga alisema watu hao walisombwa na maji umbali wa
kilometa moja huku msaidizi wa opareta wa mitambo, alikutwa amenasa kwenye miti
huku amekufa.
Dereva alikutwa amekufa umbali wa kilometa moja baada ya
kugunduliwa na wanafunzi wa shule za msingi waliokuwa wakirejea nyumbani kutoka
shuleni.
Kwa hisani ya Father Kidevu blog
No comments:
Post a Comment