ASKARI Polisi wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya , amekufa
baada ya kushambuliwa kwa kupigwa vichwa viwili na mmoja wa wateja wa baa ya
Uzunguni wilayani humo juzi usiku.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Anacleti Malindisa
alimtaja askari aliyeuawa ni Konstebo Ambros aliyekuwa na askari wenzake katika
baa hiyo, kabla ya kushambuliwa na mtuhumiwa Nurdin Juma.
Akizungumzia tukio hilo ,
Malindisa alidai Juma aliwasili katika baa hiyo saa nne usiku ambapo alivua
nguo zake zote, kubaki uchi wa mnyama na kuanza kupiga mateke viti
vilivyokuwamo katika baa hiyo.
Alisema wakati akiendelea na shughuli ya kupiga viti mateke,
ghafla alimvamia Ambros na kumshambulia kwa kumpiga vichwa viwili ambapo
alianguka chini na kwamba askari wenzake walimchukua na kumkimbiza katika
Hospitali ya Wilaya ambako alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
Kaimu Kamanda alisema, wanamshikiliwa Juma na kwamba
uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amelewa na kwamba
uchunguzi zaidi unaendelea kuhusu tukio hilo .
Kadhalika alisema mipango ya kuusafirisha mwili wa marehemu
kwenda kwao mkoani Morogoro kwa ajili ya maziko inaendelea.
Source: Habari Leo.
No comments:
Post a Comment