UTEKELEZAJI wa mpango wa CCM uliolenga kuwashinikiza
watuhumiwa wa ufisadi kuachia nafasi zao za uongozi ndani ya chama hicho,
umechukua sura mpya na sasa Kamati Kuu (CC) inaomba ipewe kibali cha
kuwachukulia hatua zaidi wale ambao wamegoma kujiuzulu.Juzi, katika kikao chake
mjini hapa, CC iliazimia kuomba idhini ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ili
ifanye kazi hiyo baada ya kuwepo ukimya ambao unaashiria kutokuwepo viongozi na
makada ambao wako tayari kujiuzulu nyadhifa zao kwa hiari.
Tangu kupitishwa kwa mpango huo maarufu kwa jina la kujivua
gamba katika kikao cha NEC kilichopita cha Aprili mwaka huu, ni kada mmoja tu,
Rostam Aziz aliyechukua hatua za kujiuzulu ubunge wa Jimbo la Igunga na ujumbe
wa NEC, lakini wengine wamekuwa kimya hadi sasa.
Katika kikao cha Aprili NEC hiyo ya CCM ilipitisha maazimio
26 lakini kubwa ni lile lililokuwa likihimiza vita dhidi ya ufisadi kuendelea
na kutoa mwito kwa watu wanaotajwa na jamii kuhusika na ufisadi ambao wako
ndani ya chama kujitathmini kisha kuchukua hatua za kuachia madaraka waliyo
nayo.
Sehemu ya mwisho ya azimio hilo inasomeka: “Wasipoachia madaraka chama
kiwachukulie hatua mara moja.”
Mmoja wa wajumbe wa CC ambaye ameomba jina lake kuhifadhiwa
alisema: “Tunawaomba NEC waturuhusu jambo hili tulifanyie kazi sisi (CC) na
litafanyiwa kazi kupitia taratibu za kawaida za chama kwa kuzingatia kanuni na
taratibu za maadili za chama hicho.”
Kubadilika kwa utaratibu wa kuwashughulikia watuhumiwa wa
ufisadi, kulipokewa kwa shangwe na wafuasi wa watuhumiwa hao ambao wanasema
kulikuwa na ajenda ya siri, kubwa likiwa ni vita ya urais wa 2015.
Hata hivyo, kada mwingine ambaye yuko karibu wa vigogo wa
chama hicho alisema: “Hivi sasa hali itakuwa mbaya zaidi kwa watuhumiwa,
tunakokwenda si hiari tena itakuwa ni lazima ikiwa chama kitawapata na hatia.”
“Ujue azimio la kwanza lilikuwa na pande mbili, kwanza ni
watuhumiwa hao kujipima wenyewe kisha kuchukua hatua, lakini pili ni upande wa
chama, sasa ukomo wa upande wa kwanza ambao ni kuchukua hatua wenyewe
umekwisha, sasa ni zamu ya upande wa pili ambao ni wa chama,” alisema kada huyo
ambaye pia ni mshiriki wa vikao vya uamuzi ndani ya CCM.
SOURCE: Mwananchi
No comments:
Post a Comment