JELA NI MAHALI PA KUISHI KAMA SABABU YA KWENDA HUKO NI VITA DHIDI YA UONEVU, UKANDAMIZAJI WA HAKI NA UTU WA BINADAMU.
Wapendwa wapiga
kura wangu na Watanzania wenzangu.
Sina wakati mgumu
kuchukua maamuzi haya yanayotokea leo. Upendo huu nilio nao kwa watu wa Arusha
na nchi yangu ni sababu ya msingi ya maamuzi haya. Nimetishwa mara nyingi,
rafiki zangu wametishwa, jamii ya watu duni imeendelea kuishi kwa mashaka na
matisho kwa muda mrefu.
Katika mazingira
haya, nikawaza sana kuwa anatakiwa kutokea mtu mmoja jasiri atakayeweza kuona
thamani ya watu wengine. Huyo mtu anaweza kuwa wewe lakini kwa wakati huu
siwezi kumsubiri tena na nimechagua kuwa mimi nikiamini kuwa utanikuta
nikiendelea na safari ya ukombozi. Tupo wengi sana tunaotaka mabadiliko, haki na
ukweli. Hata hivyo hofu, woga na mashaka yamepoteza thamani yetu yote ya maana
ya kuishi .
Waliofungwa kwa kuonewa na kuteswa, waliokosa
chakula na kulala nje, waliokwenda hospitali na kukosa madawa, waliokosa ajira
na kipato mpaka kujikuta wametoroka familia zao, waliopoteza matumaini ya
maisha, waliopora utajiri wa nchi yetu kwa manufaa yao binafsi, walionunua haki
na sheria dhidi ya wajane na wanyonge na kuwapora vipato vyao vidogo na
mashamba yao, USIULIZE SABABU NINI!.
Nimetafakari sana
na nikatambua kuwa sababu ni mimi pale nilipokuwa kimya wakati wajane na
wanyonge wanaonewa.
NIliposikia
wengine wanaandamana kupinga uovu, uonevu, wizi, ufisadi na ukandamizaji wa
haki nikasema ni hao na wala sio mimi, kumbe nilipaswa kuwa mbele katika
harakati hizi.
Nilipoona
wenzangu hawawezi kupata matibabu nikasema mimi sio mgonjwa, nilipopata taarifa
za rafiki zangu kufungwa kwa makosa yasiyo yao, nilipoona watoto wa mitaani
wanaomba chakula, nilipoona wazee wamepoteza matumaini ya kuishi katika uzee
wao, nilipoona vijana hawana ajira, nilipoona mabinti wasichana wadogo wameamua
kufanya biashara ya ukahaba, NIKATAFAKARI,TENA NIKATAFAKARI, dhahabu zetu,
almasi yetu, Milima na mabonde yetu, Tanzaninte yetu, samaki wetu, Uranium
yetu, makaa ya mawe yetu, utalii wetu,
ardhi na kilimo chetu na zaidi utu na mahusiano yetu.
Na sasa
siwezi kukaa kimya tena. NI afadhali vita inayotafuta haki na usawa kuliko
amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mwanadamu. Na katika msingi huu hofu
na mashaka vimekosa thamani kwangu, sitamwogopa mtu yoyote, mwenye silaha
yoyote, mwenye cheo chochote na wala sitaogopa jela yoyote katika kupigania
haki, utu wa kweli katika jamii yangu. Wanafikiri wataendelea kutuogopesha kwa
sababu wana jela na silaha, wanafikiri tutaendelea kuabudu uoga, wanafikiri
wataendela kutunyanyasa bila sababu ya msingi LAKINI SISI TUNAJUA TUTASHINDA
KWA SABABU HAKI TUNAYOIPIGANIA NI MAKUSUDI YA MWENYEZI MUNGU.
Leo
nitakwenda jela kwa hiari yangu binafsi kwa siku kadhaa na si kwa NIA YA
KUJITAFUTIA UTUKUFU WANGU bali ,” JELA NI MAHALI PA KUISHI KAMA SABABU YA
KWENDA HUKO NI VITA DHIDI YA UONEVU, UKANDAMIZAJI WA HAKI NA UTU WA BINADAMU.
Kila mara
nilipotishiwa nikagundua wanaonitishia, wananitishia kwa jela na mauti. Na mimi
nikagundua na nikatambua ni afadhali kuishi miaka hamsini jela huku sababu
ikiwa ni kupinga uonevu na ukandamizaji kuliko maisha ya woga na anasa yasiyo
na kusudi katika kutetea utu na heshima ya mwanadamu mwenzangu.
Wale
mlionitishia kunipeleka jela sasa nimetangulia kwa hiari yangu na wale mliobaki
msiogope jela endeleeni kupigania ukombozi utakaoleta usawa katika nchi yenu. Watakaotubeza
na kututukana wasameheni kwani wanahitaji ukombozi wa fikra, watakaotupongeza na
kutuonea huruma wafundisheni ujasiri na waambieni mapambano bado yanaendelea
tunahitaji umoja wao. Nitarudi mapema.
MSIOGOPE, MSIOGOPE, MSIOGOPE ,
MUNGU YUPO UPANDE WETU.
Mhe
Godbless Lema (MB) – Arusha Mjini
31 Oktoba 2011.
No comments:
Post a Comment