Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki- Moon kwenye Makao Makuu ya Umoja Mataifa jijini New York nchini Marekani.
|
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amepokea Tuzo Mbili Maalum kwa mchango wake mkubwa katika Afya ya Mama Mjamzito na Watoto kwa ujumla kutoka taasisi mbili tofauti mjini New York.
Tuzo ya kwanza imetolewa na Taasisi ya Kijamii ya Umoja wa Mataifa (UN Foundation) na kukabidhiwa kwa Rais na Makamu wa Rais wake anayeshughulikia sera ya Umma Bw. Peter Yeo.
Rais amepokea Tuzo ya pili katika makao makuu ya Soko la Hisa la Marekani (National Association of Securities Dealers Automated Quotations) kwa kifupi NASDAQ ambalo ni soko la pili kwa ukubwa duniani baada ya lile la New York. Rais amekabidhiwa tuzo hiyo na Makamu wa Rais wa NASDAQ Bw. David Wicks.
Mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Rais amepewa heshima maalum ya kugonga kengele kuashiria mwisho wa biashara kwa siku hiyo.
Akipokea tuzo hizo mbili maalum, Rais ameelezea changamoto zinazoikabili sekta ya Afya nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla na kuzishukuru nchi na taasisi mbalimbali ambazo zinaunga mkono juhudi za kupunguza matatizo ya afya ya mama mjamzito.
“Si sahihi kwa mama mjamzito kufariki wakati anampa uhai binadamu mwingine, uzazi unatakiwa kuwa shughuli ya furaha na sio huzuni na ndiyo maana tumetoa kipaumbele kwenye afya ya mama mjamzito kwenye ajenda yetu ya Afya” Rais amesema.
Rais amewaeleza wageni waalikwa ambao katika hadhara zote mbili wametoka katika nchi na taasisi mbalimbali kuwa kati ya vitu ambavyo serikali ya Awamu ya Nne imeamua kutoa kipaumbele katika kuongeza huduma za afya ya uzazi kwa kujenga zahanati na kuzipandisha daraja zilizokuwepo.
Serikali pia inaajiri wakunga na wataalamu zaidi wa Afya na kuongeza mafunzo katika sekta hiyo.
Juhudi zingine ni pamoja na kutoa huduma za Mpango wa Uzazi bure na kutoa vifaa vya kujifungulia kwa akina mama wanaohudhuria kliniki.
“Vifaa hivi ni maalum kwa ajili ya kuwasaidia akina mama wakati wa kujifungua, na tuna amini kuwa kwa kufanya hivi wanawake wengi zaidi watahudhuria kliniki na kuwapa motisha wa kujifungulia katika taasisi zetu za afya”. Rais ameeleza.
Kutokana na juhudi hizo takwimu zinaonyesha kupungua kwa vifo vya akina mama wajawazito na wakati wa kujifungua kutoka 8,000 kwa mwaka 2005 hadi 6,000 mwaka jana.
“Upungufu wa vifo 2,000 ni hatua nzuri katika muda mfupi lakini bado hairidhishi sana, tunaweza kupunguza zaidi na hilo ndiyo lengo letu kwani hatutaki kuona mwanamke yeyote anakufa kutokana na ujauzito au wakati wa kujifungua”. Rais amesema.
Mbali na shughuli hizo, Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Slovenia Dr. Danilo Turk, Makamu Waziri Mkuu wa Luxembourg Bw. Jean Asselborn na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki Moon na Waziri wa Maendeleo wa Uingereza Bw. Andrew Mitchell.
Leo tarehe 22 Septemba, 2011, Rais anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
MWISHO.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
New York.
Marekani.
22 Septemba, 2011
No comments:
Post a Comment