Katibu mkuu wa CCM, Wilson Mukama akitoka
kuangalia nyumba ya Katibu wa chama hicho kata ya Nyandekwa Jimbo la Igunga,
Hamis Makala iliyochomwa moto usiku wa kuamkia juzi na watu wasiojulikana.
Picha na Daniel Mjema
MATUKIO ya hujuma yanazidi kulitikisa Jimbo la Igunga safari hii watu wasiojulikana wamechoma moto nyumba ya Katibu wa CCM, Kata ya Nyandekwa usiku wa kuamkia juzi.
Tukio hilo linahusishwa na wafuasi wa Chadema kutokana na ujumbe wa maandishi uliokutwa umechomekwa katika nyumba hiyo ukisomeka: “Chadema sisi ni wajanja”.Katibu huyo, Hamis Makala alimweleza Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama aliyemtembelea jana kumpa pole kuwa, kwa muda mrefu amekuwa akiwindwa na wafuasi hao wa Chadema.
Alidai kuwa sababu ya kuwindwa na wafuasi hao inatokana na kukasirishwa na kampeni anazozifanya katika kata hiyo zinazoifanya CCM ikubalike kwa wananchi na kukiacha Chadema kikikosa watu kinapokwenda kufanya mikutano ya hadhara. Nyumba iliyoteketezwa kwa moto ilikuwa ikitumiwa na katibu huyo kwa shughuli za jiko na kuhifadhia kuku.
“Niliposhtuka na kutoka nje nilikuta moto mkubwa unawaka nikapiga yowe kuomba msaada. Lakini majirani walishindwa kuuzima kwa kuwa ulikuwa umesambaa… kuku 15 kati ya 21 waliokuwamo ndani wamekufa,” alisema.
Alisema baada ya kushindwa kuuzima moto huo na nyumba hiyo kuteketea, aliamua kulala na asubuhi majirani walipofika tena kumjulia hali ndipo walipogundua karatasi ikiwa na ujumbe wa Chadema kuhusika.
Alidai kuwa mbali na ujumbe huo, upo mwingine wa maandishi ambao ulipenyezwa katika Ofisi ya CCM ya kata hiyo unaosisitiza kuwa Chadema hawahitaji bendera za CCM katika kata hiyo. Alisema kuwa karatasi zote hizo mbili zimechukuliwa na polisi.
No comments:
Post a Comment