Barrick yawakodia wabunge ndege kwenda Nyamongo |
HATUA ya uongozi wa mgodi wa North Mara Barrick uliopo Nyamongo, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara kukodi ndege tatu ndogo kwa ajili ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kwenda mgodini hapo, imezua malalamiko huku baadhi ya wananchi wakidai kwamba kitendo hicho huenda kikashawishi mtizamo wa kamati hiyo.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, James Lembeli jana ilifanya ziara ya siku moja mgodini Nyamongo ikitokea mjini Dodoma, ziara ambayo kwa mujibu wa Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel ililenga kukagua utekelezaji wa maelekezo yake iliyoyatoa mwaka jana kuhusu athari za mazingira zilizosababisha baadhi ya wakazi wanaouzunguka kupata athari za kiafya.
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine alikuwa amealikwa kuambatana na kamati hiyo, lakini safari yake iliishia Uwanja wa Ndege wa Mjini Dodoma baada ya kubaini kwamba ndege husika zilikuwa zimekodiwa na kampuni ya Barrick.
"Kweli mimi nipo Dodoma, nimerudia pale Airport (Uwanja wa Ndege), siwezi kwenda kuwasaliti wananchi wangu wa Tarime, maana kama tunakwenda kuwakagua Barrick halafu tupande ndege za Barrick sidhani kama tutatenda haki," alisema Nyangwine alipozungumza na gazeti hili kwa simu na kuongeza:
"Barrick ndiyo (kampuni) inayotuhumiwa na wapiga kura wangu kwa kuwanyanyasa kwa kutowalipa baadhi yao fidia za mali zao hadi sasa mbali na kuhamishwa maeneo yao, kumekuwa na madhara makubwa kwa wananchi kutokana na matumizi ya maji yenye kemikali za sumu kutoka mgodini na maji hayo yanaingia Mto Tigite na kuleta madhara pia kwa wanyama, halafu nipande ndege yao! Haiwezekani."
Msimamo wa Nyangwine unafanana na ule ambao umewahi kutolewa na Lembeli katika moja ya vikao vya Bunge mwaka 2009, akisema kwamba amekataa kupanda ndege za kampuni hiyo kwani huweka gharama za safari hizo kama sehemu ya huduma inazotoa kwa jamii.
Lakini jana, Lembeli aliwaongoza wabunge wenzake kupanda ndege za Barrick ambazo zilitua Dodoma majira ya asubuhi na ujumbe wa baadhi ya wakuu wa kampuni hiyo, walioongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Deo Mwanyika kisha kuruka kuelekea Nyamongo.
"Kilichonishtua ni kumwona yule bwana Mwanyika na hapo nilimwuliza Mwenyekiti (Lembeli) kwamba hii siyo rushwa? Lakini yeye akanijibu kwamba siyo rushwa kwa sababu ni jambo ambalo limefanyika kwa uwazi, lakini mimi nikaona kwamba siwezi kwenda na kamati hiyo kwa sababu hapo hakuna uhuru wa kufanya kazi," alisema Nyangwine.
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment