MWANASIASA Mkongwe nchini Kingunge Ngombale Mwiru, ameendelea kuung'ang'ania waraka wa Kanisa Katoliki na sasa amelitaka kanisa hilo limwombe radhi kwa kumwita fisadi alipoupinga bungeni.
Waraka huo uliotolewa Machi mwaka huu, ulilenga kuwapa mwongozo waumini wa Kanisa Katoliki wa namna ya kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao, vipaumbele vya kitaifa na aina ya kiongozi anayefaa kuchaguliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, Kingunge alisema alishangaa kusikia kanisa hilo likisema wanaohofia waraka huo ni mafisadi baada ya yeye (Kingunge) kutoa angalizo bungeni katika Mkutano wa 16 uliomalizika Julai 31 mwaka huu.
"Maaskofu wamenisikitisha sana katika hili. Hatuwezi tukakubali nchi ikapelekwa wanavyotaka wao, tunaomba waache," alisema Kingunge na kuongeza:
"Nashangaa, askofu mzima akazungumza na kuniita fisadi, hiyo ni dhambi. Askofu huyo akaungame. Mimi sipendi neno fisadi ni afadhali kama rushwa iitwe rushwa".
Hata hivyo, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Method Kilaini jana alikataa kujibu kauli hiyo ya Kingunge akisema hataki kulumbana na mkongwe huyo wa siasa.
"Sitaki kulumbana naye, mzee wa watu ni mzee wa watu tu, hivyo sitaki kuendeleza malumbano naye,"alisema Kilaini.
Kwa mujibu wa Kingunge, viongozi wa Kanisa Katoliki wamemkejeli na kumtukana kuwa hajasoma kwani anaamini kwamba aliusoma waraka huo vizuri na kuulewa kwa kina kabla hajatoa kauli hiyo.
'Niliusoma vizuri na kuelewa. Hivi nitashindwa kuelewa walichoandika, nimesoma maandiko ya dini ya Kiislam, Kihindu na nyingine, siwezi kushindwa kusoma na kuelewa waraka huu." alisema Kingunge juzi alipokuwa akihojiwa na kituo cha Channel 10 na kuongeza:
"Sikutaka kuingia katika maudhui, maana nikiingia katika maudhui ningelumbana nao kwamba dini inakuaje na ilani, ilani inapaswa kuandaliwa na vyama vya siasa tu na si vinginevyo," alisisitiza.
Kingunge alisema ni vizuri kanisa likaelewa kuwa lenyewe sio chama cha siasa na kwamba, halina uwezo wa kuandaa ilani ya uchaguzi.
Alifafanua kwamba, wakati anazungumzia waraka huo bungeni hakuwa anataka uhasama na kanisa kwa kuwa anaheshimu imani, ila alikuwa akitoa angalizo kwa kuwa dini haiongozi nchi kama serikali.
"Ukiona vyaelea, jua vimeundwa" angekuwepo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hapa, kanisa hilo lisingethubutu kuandaa waraka huo, mimi pia ni mkongwe, hivyo hakuna yeyote ambaye anaweza kusimama na mimi kuhusu historia ya nchi hii.
Nataka niwaambie kwamba, tunajua mambo ya Kanisa Katoliki, lakini kwa bahati mbaya mwalimu hayupo,"alisema.
Kingunge aliendelea kulishambulia kanisa hilo akidai kuwa linataka kuwatoa Watanzania katika utamaduni wao na kulishauri kuunda chama cha siasa kama linaona ni vyema.
Alisisitiza kuwa dini si chombo cha kuunganisha watu, bali kuwatenganisha ndiyo maana kila mtu ana dini yake, lakini serikali ni moja, hivyo nchi yenye dini nyingi haiwezi kuunganishwa na dini bali siasa.
Katika malumbano hayo yaliyodumu kwa muda sasa, kanisa liliutetea waraka huo likisema kuwa sio mara ya kwanza kuutoa kwa waumini wake.
Lilisema huu umekuwa utaratibu wa kanisa hilo tangu mwaka 1995 ukiwa na lengo la kuwaelimisha waumini wake kuhusu namna ya kutekeleza haki yao ya kupiga kura.
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment