WATOTO wawili wa viongozi wa zamani wa Uganda na Tanzania jana waliandika historia mpya baada ya kukutana kwenye kijiji cha Butiama alikozaliwa na kuzikwa Rais Julius Nyerere na kukubaliana kuanza umoja mpya.
Watoto hao, Madaraka Nyerere na Jaffar Amin, ambao baba zao walionekana kuwa mahasimu wakubwa katika vita vya mwaka 1978 baina ya nchi hizo mbili, walionyesha kusikitikia vita hiyo, huku mtoto wa Idd Amin wa Uganda akisema "ilisababisha maafa makubwa" kwa wananchi wa Tanzania na Uganda.
"Vita ile ilisababisha maafa makubwa kwa wananchi," alisema Jaffar akionekana kusikitikia kitendo cha baba yake ambaye alikuwa chanzo cha vita hiyo kwa kuishambulia Tanzania kabla ya Nyerere kuamua kujibu mapigo kwa kuiondoa serikali yake madarakani.
"(Nyerere) ametuonyesha umoja, huyu ni bingwa wa suala hili. Mimi sijui kabila lolote hapa Tanzania. Najua nyinyi wote ni Waswahili, lakini kule kwetu wakiona wewe ni mrefu watasema ni kabila fulani, wakiona mweupe kidogo, mwembamba watasema wewe ni Mnyankole.
"Lakini tangu wanajeshi wenu walipokuja kwetu, mnamwita kila mtu Mganda."
Jaffar, ambaye alikuwa akizungumza lugha ya Kiswahili, akiwa amevalia kanzu ya bluu likiwa kama vazi la mitindo ya nchi za Afrika magharibi, alitaka mkutano huo, ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), baina yake na Madaraka uwe mwanzo wa mshikamano baina ya wananchi wa Tanzania na Uganda.
Mtoto huyo wa Idd Amin alienda kwenye kaburi alilozikwa Nyerere na pia kutoa zawadi ya mkeka kwa mke wa muasisi huyo wa taifa la Tanzania, Mama Maria Nyerere.
Naye Madaraka alisifu mkutano huo akisema umeongeza nia ya kuleta umoja.
Vita huyo ilidumu kwa miezi kadhaa na kufuatiwa na hali ngumu ya kiuchumi kwenye nchi zote mbili, Tanzania ikitangaza kujifunga mkanda kwa miezi 18 huku Uganda ikifuatiwa na mapinduzi mfululizo yaliyofikia ukomo mwaka 1986 wakati Rais Yoweri Museveni alipoingia Ikulu akitokea msituni.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment