JK akisalimiana na Maura Mwingira, mmoja ya maafisa ubalozini. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete Jumapili amewasili New York, Marekani kuhudhuria Kikao cha 66
cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) na kushiriki katika mikutano mingine
ya viongozi wa nchi na Serikali yenye maslahi kwa Tanzania na Afrika.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, Mheshimiwa Rais Kikwete
asubuhi ya leo, Jumatatu, Septemba
19, 2011, atashiriki mkutano wa ufunguzi wa UNGA wa viongozi wa nchi na
Serikali utakaojadili “Jinsi ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyokuwa ya
Kuambukiza (Prevention and Control of Non-Communicable Disease) ambayo ndiyo
mada kuu ya majadiliano ya Baraza Kuu la UN mwaka huu.
Rais Kikwete
leo pia atakuwa Mwenyekiti wa
mkutano wa waandishi wa habari kuhusu Maendeleo ya Umoja wa Viongozi wa Afrika
Kupambana na Malaria (African Leaders Malaria Alliance - ALMA) ambao yeye ni
mwenyekiti.
Pamoja naye katika mkutano huo, miongoni mwa waalikwa
wengine, watakuwa marais Paul Kagame wa Rwanda na Goodluck Jonathan wa Nigeria,
na Rais wa zamani wa Marekani Mheshimiwa Bill Clinton.
Rais Kikwete
pia leo atashiriki katika Mkutano wa Mwaka wa Taasisi ya Rais Clinton ya
Clinton Global Initiative, na atahudhuria mkutano maalum wenye mada ya Putting
Teeth into Non-Communicable Disease unaondaliwa kwa pamoja na Tanzania,
Australia na Sweden.
Baadaye jioni atakuwa msemaji mkuu katika hafla ya viongozi
ya nchi na Serikali kusheherekea mafanikio ya muongo uliopita ya kupambana na
ugonjwa wa malaria ulioandaliwa na taasisi ya Roll Back Malaria. Miongoni mwa
watakaohudhuria halfa hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa UN, Mheshimiwa Asha Rose
Migiro.
Jumanne,
Septemba 20, 2011, Rais Kikwete atashiriki katika mkutano wa viongozi wa nchi
na Serikali kuhusu Lishe na baadaye mchana atajiunga na Katibu Mkuu wa UN,
Mheshimiwa Ban Ki Moon kushiriki katika hafla ya viongozi iitwayo “Every Woman,
Every Child Leaders Event”. Mchana, Mheshimiwa Rais Kikwete atashiriki katika
tukio maalum la kujadili mikakati ya kimataifa kuhusu afya ya akinamama na
watoto ya Global Strategy for Women’s and Children’s Health.
Asubuhi ya Jumatano, Septemba 21, 2011, Rais Kikwete
atashiriki katika ufunguzi wa majadiliano ya mada kuu ya UNGA mwaka huu, pia
atashiriki katika mjadala kuhusu hali ya chakula wa Beyond Food Security, na
vile vile atashiriki katika mkutano wa viongozi wa Social Good Summit ambako
atapewa tuzo maalum kutoka Umoja wa Mataifa kwa mchango wake mkubwa wa
kuimarisha afya ya akinamama na watoto.
Baadaye mchana, Rais Kikwete atashiriki katika chakula cha
mchana kilichoandaliwa na Mheshimiwa Ban Ki Moon kwa ajili ya viongozi wote
wanaoshiriki katika mkutano wa 66 wa UNGA, na pia atashiriki katika tukio
jingine kuhusu afya ya akinamama lililoandaliwa na Soko la Mitaji la NASDAQ.
Baadaye jioni ya siku hiyo atahudhuria hafla iliyoandaliwa
na Rais Barack Obama wa Marekani kwa ajili ya viongozi wanaoshiriki mkutano wa
mwaka huu wa Baraza Kuu la UN.
Asubuhi ya Alhamisi, Septemba 22, 2011, Rais Kikwete
atahutububia UNGA akiwa msemaji wa pili wa siku hiyo baada ya nchi ya Cyprus,
shughuli ambayo itafuatiwa na shughuli nyingine nyingi za mikutano na viongozi
ukiwamo ule wa kuadhimisha miaka 10 ya Azimio la Durban kuhusu ubaguzi wa
rangi. Ijumaa, Septemba 23, 2022, Rais Kikwete atashiriki katika mkutano wa
viongozi wa nchi na Serikali juu ya usalama wa nguvu za nyuklia wa Nuclear
Safety and Security.
No comments:
Post a Comment