BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wana nia kugombea urais mwaka 2015, wameelezwa kukidhoofisha chama hicho kutokana na kufanya vitendo vinavyozidisha mgawanyiko ndani ya chama hicho, ikiwemo ‘kuwashughulikia’ wanachama jasiri wanaojitokeza kueleza upungufu wao ndani ya vikao.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM), Mrisho Gambo, ambaye hivi karibuni alitangazwa kusimamishwa ujumbe wa Baraza la Vijana Mkoa wa Arusha, amesema miongoni mwa hao wanaotaka urais, wanatumia mbinu chafu kuwaziba midomo wanaojitokeza kusema ukweli hadharani.
Alijitolea mfano wake yeye kuwa mwanachama mmoja mwenye nia ya urais, ameutumia Umoja wa Vijana mkoani Arusha kuitisha kikao cha Baraza Kuu kwa lengo la kumjadili yeye baada ya kutoa maoni yake kuwa watuhumiwa wa kashfa ya Richmond na Dowans ndiyo wamefanya wananchi waichukie CCM.
“Lengo la baadhi ya watu hawa wanaoutaka urais ni kutumia mbinu za kuwatisha watu wasiseme ukweli. Kwa mfano mimi nilitumia vikao vya chama kutoa kero ninayoona kuwa inaidhoofisha CCM, lakini hoja hiyo haikuwafurahisha…baadhi ya watu sasa wameitumia UVCCM kunishughulikia. Hii ni mbinu chafu kuwatisha wanachama wengine wasithubutu kusema ukweli,” alisema Gambo.
Gambo aliyetamba kuwa Baraza hilo la Mkoa halina ubavu wa kumsimamisha ujumbe wake wa Mkoa na Taifa, alishauri wanachama wanaoutafuta urais wasitumie njia ambazo zinakidhoofisha chama; badala yake wamsaidie Rais Jakaya Kikwete kuimarisha chama hicho.
“Wanaoutaka urais wamsaidie Rais kuhakikisha Ilani ya CCM inatekelezwa ili wakipitishwa kugombea iwe rahisi kwao kunadiwa; badala ya kutumbia mbinu chafu kama hii ya kutaka kuwanyamazisha watu wanaosema ukweli,” alisema Gambo....
source: HabariLeo
No comments:
Post a Comment