April 8, 2010

Mgombea Binafsi RUKSA?????

Serikali leo inatarajiwa kutoa sababu za msingi za kupinga mgombea binafsi kwenye Mahakama ya Rufaa ambako ilikata rufaa maamuzi ya Mahakama Kuu kuruhusu mgombea binafsi katika kesi iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa chama cha Democratic Party (DP) Christopher Mtikila.

Serikali ilikata rufaa Mahakama ya Rufaa mwaka jana ikipinga hukumu ya Mahakama Kuu Dar es Salaam iliyotolewa Mei 5 2006 katika kesi ya msingi namba 10 ya mwaka 2005 iliyofunguliwa mahakamani hapo na Mchungaji Mtikila Februari 17 mwaka 2005 akiiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru kuwepo kwa mgombea binafsi.

Katika hukumu hiyo jopo la majaji watatu wa mahakama Kuu Dar es Salaam, jaji Amir Manento, jaji Salum Massati na jaji Thomas Mihayo, wakati huo walikubaliana na maombi ya Mchungaji Mtikila na kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi.

Hata hivyo serikali ilikata rufaa Mahakama ya Rufaa, ambayo ilitarajiwa kusikilizwa Februari 8 mwaka huu lakini iliahirishwa hadi leo baada ya serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali(Dag), George Masaju kuomba iahirishwe ili ipate muda zaidi wa kujiandaa katika kutoa hoja zake.

Wakati muda huo serikali ilipewa kujiandaa zaidi ukiwa ndio umemalizika na leo inakuja tena mahakamani, mahakama hiyo nayo kwa upande wake imekuwa ikichukua hatua madhubuti za kujiimarisha kujiongezea nguvu zaidi kwa kutafuta msaada zaidi wa kisheria kutoka kwa watalaamu wa mambo ya Katiba na sheria kwa jumla.

Jambo kubwa la kuvutia wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo ni kwamba leo itasikilizwa mbele makundi mawili yenye majopo ya majaji tofauti na awali kabla ya kuahirishwa.

Majopo hayo ni pamoja na jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa na jopo la wataalamu watatu wa sheria, wasio majaji wala mawakili, ambao kwa lugha ya taaluma ya sheria hujulikana kama marafiki wa mahakama (Friends of Court).

Jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa katika rufaa ya kesi hiyo hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu mwenyewe Ramadhani ambaye ndiye kiongozi wa jopo la majaji hao akisaidiana na Jaji Eusebio Munuo, Jaji Januari Msofe, Jaji Benard Luanda, Jaji Mbarouk Mbarouk, Jaji Engela Kileo na Jaji Sauda Mjasiri.

Kwa upande wa jopo la marafiki wa mahakama ambao tayari wameitwa na mahakama hiyo kushiriki kwenye rufaa ya kesi hiyo ni pamoja na Profesa Kabudi Palamagamba na Profesa Jwani Mwaikusa ambao wote ni wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa (UDSM).

Pamoja na maprofesa hao wawili wa UDSM, mwingine katika jopo hilo ambaye pia ameitwa na mahakama hiyo kushiriki katika usikilizwaji wa rufaa ya kesi hiyo ni Mkurugenzi wa mashtaka wa Zanzibar Othmani Masoud.

Katika barua za kuwaita kushiriki katika rufaa ya kesi hiyo Jaji Mkuu Ramadhani alisema ameamua kuwaita kushiriki katika kesi hiyo kutokana na umuhimu wa suala hilo kikatiba na kwamba kwa uzoefu wao katika mambo ya kisheria anaamini kuwa Mahakama hiyo itafaidika sana na ushauri wao kutokana na uzoefu wao katika mambo ya kikatiba.

Hoja ya kuwepo kwa mgombea binafsi imekuwa ikiungwa mkono na wadau mbalimbali wa siasa na utawala bora wakidai kuwa uamuzi huo utazidi kupanua wigo wa demokrasia nchini.

Jaji Mkuu Ramadhani pia kwa upande wake amewahi kukiri kuwa suala hilo lina umuhimu wa pekee na kwamba ni kutokana na umuhimu huo ndio maana aliamua kuteua jopo la majaji saba kusikiliza rufaa ya kesi hiyo.

SOURCE: MWANANCHI

No comments:

Google+ Followers

Arts n' Photo sildes

"SILENT VOICES" PHOTO EXHIBITION

Future Stars!

Some of published work

RIGHT TO BE RICH

RIGHT TO BE RICH
The ownership of money and property comes as a result of doing things in a certain way, and those who do things in this certain way — whether on purpose or accidentally — get rich, while those who do not do things in this certain way — no matter how hard they work or how able they are — remain poor. WDW Do things in RIGHT way now, but how? Call: +255716927070/+255784475576

Popular Posts

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...