KAMATI ya Bunge ya Ulinzi na Usalama imeeleza kutofurahishwa na kauli tata zinazotolewa kuhusu ajali ya gari aliyopata mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe, ikisema zinaweza kuvuruga amani na utulivu wa nchi.
Onyo hilo lilitolewa wakati kamati hiyo ikipokea taarifa ya matukio ya ajali mbalimbali nchini, ikiwemo ya mbunge huyo liyotokea mkoani Iringa wakati akisafiri kutoka Mbeya kuja Dar es salaam katikati ya mwezi uliopita.
Tahadhari hiyo ya kamati ya bunge imekuja wakati tayari kumekuwepo na mvutano kuhusu mazingira halisi ya ajali hiyo iliyotokea Makambako, Iringa.
Mkanganyiko uliopo hadi sasa ni kuhusu kauli mbili tofauti za Jeshi la Polisi, moja ikiwa imetolewa katika ripoti ya matokeo ya uchunguzi na nyingine ikisema ripoti halisi haijatoka, huku maelezo ya ajali hiyo yaliyotolewa na polisi yakitofautiana na ya Dk Mwakyembe.
Akizungumzia mkanganyiko huo jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Wilson Masilingi, ambaye ni mbunge wa Muleba Kusini kwa tiketi ya CCM, alisema taarifa waliyopokea kutoka polisi inaonyesha ajali hiyo ni ya kawaida kama zilivyo nyingine.
"Tumepokea taarifa ya matukio ya ajali nchini, ikiwemo zinazohusiana na baadhi yetu sisi wabunge. Kuna hii ya Dk Mwakyembe ambayo polisi wanasema ni ya kawaida kama ajali nyingine tu," alisema Masilingi.
No comments:
Post a Comment