February 21, 2008

Wana Jambo Forum kulikoni?

Wafichua ufisadi kwenye mtandao wahojiwa Polisi. WAMILIKI wa mtandao wa kompyuta ujulikanao kama Jambo Forum ambao umekuwa mstari wa mbele wa kuendesha mjadala juu ya madai ya ufisadi serikalini, wamekamatwa na kuhojiwa na Polisi, kwa madai ya kukashifu na kufanya uchochezi. Mkuu wa Polisi Inspekta Jenerali Said Mwema alithibitisha jana kuwa wanaendelea kuwahoji watuhumiwa wawili, kwa kile alichokieleza kuwa ni kujihusisha na uhalifu wa mtandao wa kompyuta. Alisema baadhi ya watu wanaojadiliwa kwenye mtandao huo ambao wanahusishwa na tuhuma za ufisadi, ndiyo walioulalamikia mtandao huo kuwa unatumika kuwakashifu na kuchochea hasira za wananchi dhidi yao. Mtandao wa Jambo Forum (JF) umekuwa maarufu nchini kutokana na watu wengi kutoa maoni yao katika matukio mbalimbali yanayotokea nchini. Masuala ya ufisadi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kashfa ya Richmond ni mambo ambayo yamekuwa yanatawala mjadala kwenye mtandao huo. Katika siku za karibuni mtandao huo umekuwa na mjadala mpana kuhusu waliojiuzulu serikalini na kutajwa bungeni baada ya kuhusishwa na kashfa ya Richmond. Mwema alikataa kuwataja watuhumiwa hao, lakini gazeti hili limebaini kuwa waliokamatwa na kuhojiwa na Polisi ni Maxence Melo na Mike Mushi, wote wakazi wa Dar es Salaam. Vijana hao ndiyo wanaomiliki mtandao huo ambao pia unachangiwa maoni na wananchi mbalimbali, wakiwamo waandishi wa habari na watu wengine maarufu. Mwema hakueleza uchochezi waliofanya au kashfa waliyoitoa watuhumiwa hao kupitia mtandao wa Jambo. “Baadhi ya taarifa zimeonekana kuwa za uhalifu, kukashifu na uchochezi. Polisi inatambua na kuheshimu uhuru wa katiba wa kila mtu kutoa maoni na mawazo yake na litaendelea kufanya hivyo. Lakini hakuna uhuru usiokuwa na mipaka,” alisema. Mwema alisema uhuru huo usitumike kama kivuli cha kuhalalisha utendaji wa uhalifu. Alisema sheria za nchi zinazoruhusu utoaji wa maoni uzingatiwe na kila mtu. Alisema itakapobainika uvunjaji wa sheria unatokana na matumizi mabaya ya mitandao, watakaohusika watachukuliwa hatua za kisheria. Baadaye DCI Manumba alisema kuna baadhi ya watu wamelalamika kwamba wanakashifiwa katika mtandao huo. Alisema kuna habari nyingi kwenye tovuti hiyo, kwa sasa wanaendelea kuchambua baadhi ya habari zinazodai kuwakashfu baadhi ya watu. “Tutashirikiana na wananchi ambao wamelalamika kuona ni habari gani za kuwakashifu na za uchochezi, kwa sasa siwezi kuzitaja habari hizo,” alisema DCI Manumba alipojibu maswali ya wanahabari. Mwanasheria wa watuhumiwa hao, Tundu Lissu, aliliambia gazeti hili jana kuwa wateja wake wamehojiwa kutokana na mijadala inayoendelea ya ufisadi nchini. Mwanasheria huyo alisema kitendo cha kuwahoji wateja wake kwa mjadala huo ni kinyume cha sheria, kwa vile mtandao ni kitu kinachotumiwa na watu wengi kutoa maoni yao kuhusiana na mjadala uliopo kwa wakati husika. Lissu alisema kwamba wateja wao wamekamatwa kuanzia juzi wakahojiwa kwa zaidi ya saa 14 kinyume cha sheria. “Wamehojiwa kwa saa14 na wameachiwa leo asubuhi (jana) kwa dhamana,” alisema. Wakati huo huo, polisi imekiri kuwa inawashikilia baadhi ya watu kwa tuhuma za kupanga vitendo vya kigaidi wakilenga kufanya mashambulizi wakati wa ujio wa Rais wa Marekani George W. Bush. Mkuu wa Polisi Mwema alisema jana kuwa polisi walikuwa na taarifa za watu hao kutokana na mienendo yao na mawasiliano waliyokuwa wanayafanya na baadhi ya watu katika nchi za Kenya na Somalia. Mwema alisema walilazimika kuwakamata watu hao kuzuia kitendo chochote cha kigadi ambacho kililengwa kufanywa na watu hao. IGP alisema hata kama wasingefanikiwa kuleta madhara katika msafara wa Rais huyo wa Marekani, wangefanya kitendo hicho sehemu yoyote. “Sisi tunaamini kuwa kama wangefanya kitendo hicho cha kigaidi sehemu nyingine kwa nia ya kuvuruga ziara hiyo ingekuwa sifa mbaya kwa taifa letu, ni kutokana na hali hiyo tumelazimika kuwakamata na tunaendelea kuwahoji,” alisema Mwema. Hata hivyo, Mwema hakutaja majina ya watu wanaoshikiliwa. Alisema baadhi wamekamatwa mjini Arusha ambako watu wanane wanawahoji wakati mjini Dar es Salaam wanashikiliwa watu wengine wawili na kufanya idadi ya watu hao kuwa tisa. Rais Bush alianza ziara nchini Jumamosi iliyopita na aliondoka juzi baada ya kutembelea mikoa ya Dar es Salaam na Arusha.

No comments:

Google+ Followers

Arts n' Photo sildes

"SILENT VOICES" PHOTO EXHIBITION

Future Stars!

Some of published work

RIGHT TO BE RICH

RIGHT TO BE RICH
The ownership of money and property comes as a result of doing things in a certain way, and those who do things in this certain way — whether on purpose or accidentally — get rich, while those who do not do things in this certain way — no matter how hard they work or how able they are — remain poor. WDW Do things in RIGHT way now, but how? Call: +255716927070/+255784475576

Popular Posts

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...