February 4, 2008

KARAMAGI

Wabunge wamgomea Karamagi Wakataa kujadili miswada mipya,
wataka ripoti ya Richmond Wasema wamechoka kuonekana mbumbumbu,
wamzomea
WAZIRI wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya wabunge kukataa kuijadili miswada ya Sheria ya Umeme na ya Biashara ya Mafuta katika semina na kumtaka aiondoe hadi watakapoiona na kuijadili ripoti ya kamati teule ya Bunge kuchunguza kampuni ya umeme ya Richmond.
Sambamba na kuikataa miswada hiyo ambayo lengo lake ni kuruhusu watu binafsi kujiingiza katika biashara ya umeme, wabunge hao ambao wengi ni kutoka CCM, walidai hawana imani na Wizara ya Madini na sasa hawatakubali tena kugeuzwa wajinga kupitisha sheria zinazoruhusu mikataba mibovu ya kuwanufaisha watu wachache.
Wamedai wizara hiyo imepoteza sifa na imani kwa wananchi na wabunge, hivyo wao si lazima waipitishe miswada hiyo pindi itakapofikishwa bungeni. Wabunge hao walitoa madukuduku yao wakati Wizara ya Nishati na Madini ilipoandaa semina jana katika ukumbi wa Bunge kuelezea miswada ya sheria ya Umeme na ya Biashara ya Mafuta.
Wabunge hao walidai wizara hiyo haikujiandaa kuelezea juu ya sheria hizo, na pia inaonyesha ina lengo la kuwanufaisha watu wachache ambao wanataka kuendesha biashara ya kutoa huduma za umeme, hali inayoonekana kuliua zaidi Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Miswada hiyo imepangwa kufikishwa katika Bunge hili la 10 linaloendelea.
Mbunge wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya (CCM), alisema hawawezi kuzungumzia miswada hiyo hadi hapo watakapojadili ripoti ya Richmond na kuomba ripoti hiyo ijadiliwe kwa hati ya dharura. “Mtu akiitwa Mbunge, ana akili nzuri. Tulishakosea kwa mara ya kwanza. Kwa mara ya pili tukikosea tena, watu watatuona sisi stupid (wajinga). Nani kaipeleka Tanesco ICU (chumba cha wagonjwa mahututi)? Tukishasoma ripoti ya Richmond kwa siku mbili ndipo tutajua huenda kuna mkono wa mtu ulioifikisha Tanesco pale. “Nasema kama Mama na Mbunge, hata utuweke hapa hadi keshokutwa au utuweke siku nne, hatutairuhusu miswada hii, wewe Waziri umekuwa na Richmond ndio unaijua sisi hatuijui, tunataka kuijua sasa”, alisema Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM).
Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni, wakati akichangia alisema; “Umefika wakati tufanye wanachotaka wananchi, Bunge kufanywa rubber stamp (mhuri) sasa umepitwa na wakati. Tumechoka kuonekana stupid (wajinga). Tuiweke pembeni miswada na tumalize yaliyopo mezani. Kuna mikataba mibovu ya Richmond, IPTL nk. Kila tulipobinafsisha tumeungua na moto, tumebinafsisha rojo rojo tu, tukishindwa kufanya wanachotaka wananchi tujiuzulu”. “…Sijui fedha za BoT zimekwenda kuunda makampuni ya kuzalisha umeme, inawezekana zimekwenda kununua majenereta… , hatupo tayari kupokea muswada mmeleta kiajabu ajabu inaonekana hata nyinyi hamjiamini mlikuwa na wasiwasi..naomba mwenyekiti funga semina yako tukutane bungeni”, alichangia Mbunge wa Longido, Michael Lekule Laizer (CCM).
Wakati wabunge hao wakieleza hayo, Mbunge wa Karatu, Dk. Willbrod Slaa (Chadema), alisema kupitishwa kwa sheria hizo kutaruhusu ubadhirifu zaidi na kutolea mfano kwa utaratibu wa mikopo ya uagizaji wa bidhaa nje (import support) katika kipindi cha mwaka 1985 hadi 1992 zaidi ya makampuni 982 yalianzishwa huku mtu mmoja akianzisha kampuni 35 na mpango huo ulisababisha upotevu wa Sh trilioni moja ambazo alidai kwa mazingira ya nchini hayaruhusu wawekezaji katika sekta za umeme. Pia aliahidi kutoa majina ya waliohusika na upotevu wa fedha hizo.
Wabunge hao walishauri muswada wa umeme kusitishwa hadi watapogundua sehemu ilipokosewa kwenye mkataba wa Kampuni ya Richmond wa zabuni ya kuiuzia umeme Tanesco pamoja na kulifanya shirika hilo pekee la umeme kuwa katika hali nzuri. Walisema shirika hilo linafanya vibaya kutokana na baadhi ya watu kulifikisha hapo, hivyo si sahihi kwa sasa likiwa lina hali mbaya liwekwe pamoja na mashirika mengine kushindana kibiashara. “Kuna uchafu mwingi Tanesco, kwanza usafishe, kuna mikono ya watu wachache kwenye miswada hii ndio maana unaona wabunge tunasita, hii ni semina tunawaambia ukweli, hatutaki kubeba matatizo zaidi…,” alisema Mbunge wa Iramba Magharibi, Juma Kilimbah Mbunge wa Musoma Mjini Vedasto Manyinyi (CCM), aliongeza; “Hapa kuna mtu anatafutiwa biashara, hatuna haja kubishana, Waziri simama sema unaahirisha miswada yako ili kesho usiumbuke na serikali yetu”.
Hata hivyo, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed(CUF), alimshauri Waziri kuiondoa miswada hiyo na badala yake ifanyiwe tathmini upya na ipitiwe kwa kina na baadaye ipelekwe bungeni na kuongeza; “Serikali isome mood (hali) za wabunge na wananchi ndipo ilete miswada”. Mbali na wabunge hao kuchangia kwa kuzungumza, Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM) alichangia kwa maandishi ambapo Mwenyekiti wa semina hiyo ambaye ni Mbunge wa Kyela, Harrison Mwakyembe, alisoma mbele ya wabunge kuwa; “…Nikipiga picha Tanzania ijayo nachanganyikiwa kuona wenye viwanda wanagonganisha glasi za waini huku serikali ikiwa houseboy, bora nife mapema kuliko kuiona Tanzania hiyo…” Kutokana na wabunge hao kukataa kuendelea kwa semina hiyo iliyokuwa na lengo la kujadili miswada hiyo, Mwenyekiti huyo alilazimika kuifunga semina saa 7:30 mchana wakati muda uliopangwa ulikuwa saa 8:00 mchana. Kwa muda wote huo, wabunge hao hawakujadili miswada hiyo licha ya kusikiliza maelezo ya utangulizi kutoka kwa Waziri na Kamishna wa Nishati, Bashir Mrindoko, pamoja na mwanasheria wa wizara hiyo.
Baada ya kumaliza kutoa dukuduku yao walikataa Waziri Karamagi kutoa maelezo yoyote mwishoni kama ilivyo kawaida na kulazimika semina hiyo kufungwa ambapo dakika za mwisho kabla ya kufungwa semina hiyo majadiliano yalikuwa hivi:
Mwakyembe: Waheshimiwa wabunge naomba sasa nimruhusu Waziri kutoa maelezo yake.
Wabunge: (Wakizomea) hatutakiiiiiiiiii, funga semina Mwakyembe: Sasa basi naomba nimruhusu Naibu waziri wake(William Ngeleja) awashukuru.
Wabunge: (Wakizomea) hatutakiiiiiiiiii
Mwakyembe: Hata yeye hammtaki ambaye mlikuwa naye karibuni tu? Wabunge: Hatutakii
Mwakyembe: Sasa basi kamati(Uwekezaji na Biashara) itakutana na Waziri Jumanne na naomba nifunge semina hii. Awali katika maelezo yake, Mrindoko, alisema kuwa kwa sasa upotevu wa umeme ni asilimia 28 wakati kiwango kinachotakiwa cha upotevu ni asilimia kati ya 12 na 13 na kuongeza kuwa katika kipindi cha miaka 25 ijayo mahitaji yataongezeka mara nane. Kwa sasa matumizi ni megawati 660.
Naye Waziri Karamagi alisema sheria ya mafuta ina lengo la kuifuta sheria ya mwaka 1981 ya mafuta ambayo ilionekana ina upungufu, ikiwemo kutoruhusu sekta binafsi kuwekeza katika biashara ya petroli, haizingatii suala la mazingira na ilikuwa na lengo la kubana au kupunguza matumizi ya mafuta.

No comments:

Google+ Followers

Arts n' Photo sildes

"SILENT VOICES" PHOTO EXHIBITION

Future Stars!

Some of published work

RIGHT TO BE RICH

RIGHT TO BE RICH
The ownership of money and property comes as a result of doing things in a certain way, and those who do things in this certain way — whether on purpose or accidentally — get rich, while those who do not do things in this certain way — no matter how hard they work or how able they are — remain poor. WDW Do things in RIGHT way now, but how? Call: +255716927070/+255784475576

Popular Posts

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...