WANAHARAKATI wa usawa wa jinsia, haki za binadamu na demokrasia, wamedai Bunge limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali kwa kuridhia kuzika masuala ya Richmond na Kiwira katika mkutano wake uliomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma.
Muungano wa Asasi za Kiraia zinazotetea Usawa wa Jinsia, Haki za Binadamu, Maendeleo ya Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi (FemAct), umetoa tamko ambalo pamoja na mambo mengine, linawataka wanaharakati hao waandamane kwa lengo la kuonesha kutoridhishwa na Bunge hilo.
Katika kile kinachoonesha ni kuibua mjadala na mgongano wa kimawazo kati yao na wabunge, wanaharakati hao wamesisitiza kwamba uamuzi wa kulinyooshea Bunge kidole, hauwezi kuwa mgogoro, kwani chombo hicho hakiko juu ya wananchi.
“Bunge haliko juu ya wananchi. Kimsingi wananchi tunataka. Huu si mgogoro, huwezi kuwa na mgogoro na mtu unayemwajibisha,” alisema mwakilishi wa Shirika la Fordia, Buberwa Kaiza na kusisitiza kwamba tamko hilo halitokani na kuwaridhisha wafadhili kama ambavyo imekuwa ikidhaniwa.
Wanaharakati hao katika tamko lao lililosomwa jana Dar es Salaam na wawakilishi wanne kwa nyakati tofauti, zaidi ya kusema Bunge halikutimiza wajibu katika taarifa zilizofikishwa katika mkutano wake wa 18, hawakuweka bayana kasoro za Bunge katika kushughulikia masuala ya Richmond, TICTS, TRL, taarifa ya uchafuzi wa mazingira kwa kemikali za sumu ulioathiri binadamu katika mgodi wa North Mara na ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo la Loliondo.
source: HabariLeo
No comments:
Post a Comment