February 26, 2008

Muslim on HIV/AIDS

Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa JAKAYA MRISHO KIKWETE katika Uzinduzi wa Mkutano wa Kwanza wa Viongozi wa Dini ya Kiislamu juu ya mapambano dhidi ya UKIMWI 26 FebruarI, 2008 Mzee wetu Mh. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili; Naibu Mufti wa Tanzania; Kadhi Mkuu, Kenya; Kadhi Mkuu, Zanzibar; Waheshimiwa Mawaziri; Waheshimiwa Mabalozi wa Marekani na Uingereza; Viongozi na wasomi wa Dini ya Kiislamu, Mabibi na mabwana, Assalaam Alaykum, Ni faraja kubwa kwangu kujumuika nanyi katika mkutano wenu huu muhimu unaozungumzia jambo ambalo linaathiri na kuwagusa watu wetu wengi na pia maendeleo yetu kama nchi. Sina budi kuwapongeza kwa dhati kwa kuamua kulijadili tatizo hili ambalo ni muhimu kwetu sote na ufumbuzi wake unahitaji mchango wa kila mmoja wetu wakiwemo viongozi wetu wa dini. Kama mnavyofahamu hii ndiyo sera ya serikali yetu. Sote tunafahamu kwamba hali ya UKIMWI kulingana na taarifa za awali za zoezi la upimaji wa hiari nililolizindua tarehe 14 Julai, 2007 hapa Dar es Salaam na kupata muitikio nchi nzima unaonesha kuwa maaambukizi ya UKIMWI nchini ni wastani wa asilimia 5. Hadi sasa watu zaidi ya milioni 3.4 ambao ni sawa na asilimia 85 ya lengo wameshajitokeza kupima virusi vya UKIMWI kwa hiari. Mbali na mafanikio yetu katika upimaji, bado UKIMWI unaendelea kuwa tishio maana unaambukiza hasa wale waliyo katika rika tunalolitegemea kama nguvu kazi ya nchi, yaani miaka 14 hadi 45, wanawake na wanaume. UKIMWI hauchagui umri, dini, wala nafasi ya mtu katika jamii; kwa mfano watoto 1,400,000 (wenye umri wa chini ya miaka 17) wamepoteza mzazi mmoja au wote kutokana na UKIMWI. Leo hii hakuna familia hata moja katika jamii yetu na wa dini zetu zote ambao hawajaathirika na UKIMWI kwa njia moja ama nyingine. Kwa mfano, kila mwaka takriban watoto 50,000 hadi 60,000 (yaani watoto 138 kila siku; 5 hadi sita kwa kila saa moja) wanazaliwa wakiwa na virusi vya UKIMWI. Hii ni kuonyesha tu ukubwa wa tatizo hili. Wataalam wanatuambia kuwa makisio ya umri wa kuishi ya Mtanzania leo hii yanakadiriwa kupungua kutoka miaka 52 kabla ya nchi yetu kukumbwa na tatizo la UKIMWI hadi miaka 37 ifikapo mwaka 2010. Kama havitapigwa vita, UKIMWI na virusi vya UKIMWI vitakuwa tishio kubwa katika fursa za taifa za maendeleo ya kiuchumi na uhai wa watu wetu kwa jumla. Leo hii mama mwenye umri wa miaka 20 ni mjane. Watoto wa umri wa miaka 5 ni yatima. Hali hii siyo nzuri hata kidogo. Uwezo wa kukabiliana na janga hili kwa Waislamu hivi sasa ni mdogo sana kutokana na kutokuwa na msimamo na mbinu za pamoja miongoni mwa viongozi na wasomi wa Kiislamu. Pia jamii ya Kiislamu inakabiliwa na wasiwasi wa kulijadili tatizo hili, au kutolikubali tatizo. Aidha, kuna ukimya, usiri na wakati mwingine kuna taarifa potofu, unyanyapaa, kunyoosheana vidole na kutofahamika nafasi ya Uislamu katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Kwa ujumla kuna ukosekanaji wa wazi wa programu za UKIMWI zinazowahusisha waumini wa Kiislamu moja kwa moja. Nafurahi kuwa nyinyi viongozi sasa mmekubali kwa pamoja kuchukua nafasi yenu katika kupambana na janga hili. Kama mnavyofahamu dini ina nafasi kubwa na imekuwa kimbilio la mwanadamu tangu enzi za utumwa na katika majanga ya asili kama njaa, mafuriko, matetemeko, vita, na sasa UKIMWI. Dini ina nafasi sio tu katika kuzuia kuenea kwa UKIMWI bali pia katika kuwatunza yatima na kuwafariji kiimani wagonjwa wa UKIMWI. Aidha, Jumuia za Kidini Tanzania zina utamaduni wa muda mrefu na wa kipekee wa kuongoza watu katika mwanga nyakati za matatizo makubwa na kuwajali waumini wake. Pia zimejithibitishia kuwa mhamasishaji mkuu wa wanaume, wanawake na watoto. Ni matumaini yangu kuwa baada ya semina hii ya leo Misikiti itakuwa imeona mwanga na kuanza kuchukua hatua mbalimbali kufikia vijana wa rika zote na wa jinsia zote. Pia nafasi hii tuitumie kuhakikisha kuwa maadili yanadumishwa yakiwemo yale tunayofundishwa kwenye msahafu kuhusu matunzo ya yatima na wajane na hatari ya dhuluma kwa makundi haya ya watu. Nimearifiwa kwamba warsha yenu inalenga kuandaa tamko la pamoja juu ya mbinu za kukabiliana na UKIMWI, kuimarisha nia thabiti ya viongozi wa Kiislamu juu ya kupambana na UKIMWI na kujiongezea uwezo wa kuendesha programu za kupambana na UKIMWI miongoni mwa jamii zenu. Hivyo muda sasa umefika kwa viongozi wa Kiislamu hapa nchini kutambua kwa kupitia tamko mtakalolitoa kwamba ni kwa kujitolea, na kutumia nguvu za akili na uthubutu wa moyo ndipo tutakapoweza kuushinda UKIMWI. Napenda kurudia kwenu kuwa Tanzania bila UKIMWI inawezekana ikiwa kila mmoja wetu atashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Kwa tamko lenu mtakuwa mnatangaza nia yenu ya kutekeleza yote yaliyo ndani ya uwezo wenu katika kutokomeza janga la UKIMWI, kupiga vita woga, unyanyapaa na kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya UKIMWI na virusi vya UKIMWI. Pia kwa tamko lenu mtakuwa mnaazimia kuendeleza programu za kuzuia UKIMWI kwa vijana wetu, kujenga ufahamu wa UKIMWI na mikakati ya kuuzuia kwa pamoja kwa kutoa ushauri nasaha na kupima. Ninafurahi kuona kuwa mmewaalika wenzetu kutoka nchi za jirani ambao nao wana harakati kama za kwetu za kupigana na janga hili la UKIMWI. Hilo ni jambo zuri kwani tunapobadilishana mawazo ndipo tunapopata ufumbuzi ambao pengine umeishajaribiwa na wenzetu na kuonekana unafaa. Hali kadhalika, nasi nina hakika tunayo mengi ambayo tumeyajaribu na yanafaa kwenye hali yetu hapa Tanzania. Wenzetu nao wanaweza kujifunza kutoka kwetu. Maana UKIMWI hauna mipaka. Mwisho, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati Waheshimiwa Mabalozi wa Marekani na Uingereza ambao wamesaidia kufanikisha mkutano huu muhimu. Tunawashukuru sana kwa mchango wao. Kwa hayo machache, nawatakia mkutano mwema, Inshallah Mwenyezi Mungu ajaalie mkutano huu utoe matunda mema ya kuwa na kauli ya pamoja inayolenga kupunguza kasi ya maambukizi mapya na pia kupunguza makali kwa wale ambao tayari wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Serikali inafanya jitihada zote ili kuhakikisha kuwa zoezi la upimaji linaendelea vizuri na dawa za bure kwa waathirika zinakuwepo. Baada ya kusema hayo sasa natamka kuwa mkutano huu umefunguliwa rasmi. Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Google+ Followers

Arts n' Photo sildes

"SILENT VOICES" PHOTO EXHIBITION

Future Stars!

Some of published work

RIGHT TO BE RICH

RIGHT TO BE RICH
The ownership of money and property comes as a result of doing things in a certain way, and those who do things in this certain way — whether on purpose or accidentally — get rich, while those who do not do things in this certain way — no matter how hard they work or how able they are — remain poor. WDW Do things in RIGHT way now, but how? Call: +255716927070/+255784475576

Popular Posts

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...