March 21, 2008

KILAINI APIGA MSUMARI WA MOTO KWA MAFISADI

  • ASEMA SI WARUDISHE TU BALI NA RIBA KAMA ZAKAYO. Leo ni siku ambayo kila mtu aaminiye katika Bwana Wetu Yesu Kristo yuko katika maombolezo kwa sababu tunakumbuka kifo chake. Katika kukumbuka kifo chake tunakumbuka dhambi zetu ambazo alikufa ili atukomboe nazo. Nabii Isaia alimwagua kama tulivyosoma katika somo la kwanza akisema kwamba ‘kama mwanakondoo achukuliwaye machinjioni, hana tena sura ya kupendeza na wala hatamaniki, anateswa lakini hafungui mdomo wake kulalamika. Anadharauliwa na kukataliwa na watu; anaonewa na kuhukumiwa lakini ananyenyekea; anapigwa kwa sababu ya makosa ya watu.’ Maneno hayo ya Nabii Isaiya yalithibitika katika Yesu Kristu. Kweli kwa ajili yetu alitimiza aliyoyahubiri kwamba hakuna aliye na upendo kuliko la yule atoaye uhai wake wa rafiki zake’ Leo somo kuu lililosomwa ni lile la mateso ya Bwana Wetu Yesu Kristu kama yalivyoandikwa na mtakatifu Yohane. Simulizi linasikitisha sana kwa sababu kwa upande mmoja linaonyesha mateso makubwa ya Bwana wetu Yesu Kristu na kwa upande mwingine lionaonyesha woga wa kutea ukweli, usaliti, ugeugeu wa binadamu na uchoyo. Bwana wetu Yesu Kristu alikufa ili tuepukane na haya yote, ili tugeuke na kuwa watu wapya, ili tuwe na uzima na tuwe nao tele. Alishinda mauti ili na sisi tusiwe tena na woga katika kutenda mema. Aliteswa sana kimwili, kihadhi, alidhalilishwa, alitukanwa, alipigwa na mwishowe kusulubiwa msalabani na kutundikwa akiwa mtupu bila nguo zake. Je kama yeye amefanya hayo yote kwa ajili yangu mimi niogope nini tena katika kutetea na kutenda mema. Tuseme kama mtakatifu Paulo baada ya kumpokea Mwokozi na kumfuata “ Bwana yuko pamoja nami sitaogopa kitu iwe njaa, mateso au kifo” Kifo chake Bwana Wetu Yesu Kristu kilipokelewa tofauti na watu mbali mbali wakati wake na katika historia; na je wewe umekipokeaje? Unafuata mfano gani kati ya wale waliojikuta naye katika wakati wake. Mtakatifu Petro alimpemda Yesu sana na kwa kweli alimpigania alivyoelewa yeye lakini alipokemewa akafa moyo hakujua upendo wa Yesu ukoje. Hata hivyo alimfuata mpaka kwa kasisi mkuu lakini akaishia kumkana kwa woga. Kwa sababu alimpenda Yesu kwa dhati aliweza kutubu na baadaye kuwa mkuu wa kanisa. Nasi tunaanguka lakini mradi tunampenda tusikate tamaa tuinuke na kufuata Mungu. Yohana mpendwa wa Yesu anafuata bila makeke au kelele mpaka saa ya mwisho na kwa niaba yetu anmuaga Bwana na kupewa mama yake. Mitume wengine wanakimbia na kujificha lakini yalipoisha wakakusanyana na kupeana moyo na kuhimizana hadi Yesu alipowatokea tena na kuwapa nguvu mpya. Mbaya wa siku ni Yuda ambaye kwa ajili ya vipande 30 vya fedha anamwuza Bwana na Mungu wake. Kwa fedha mtu anaweza kununua vitu vingi lakini hawezi kununua utulivu, furaha, amani na kwa uhakika hawezi kuupata ufalme wa Mungu. Hivyo vipande 30 vya fedha Yuda hakuvifurahia na badala yake alijitundika mtini. Tujihadhali na fedha chafu vinginevyo tutaishia kama Yuda. Tumwombe Mwenyezi Mungu katika Yesu aliyekufa ili kuushinda ubaya nasi atuepushe na tamaa ya fedha, tamaa ya utajiri na tamaa mali. Siku hizi duniani na kwa namna ya pekee hapa kwetu Tanzania tunasikia na kusoma kama kwa Yuda juu ya ubaya wa tamaa hiyo ya fedha inayoua na kuharibu. Kuna wanaobaka watoto hata wa chini ya miaka miwili ili wapate fedha. Fedha ya dhambi, ya kufuru. Fedha hawatapata ila laana tu. Kuna wanaoua waalbino eti wapate fedha. Damu hiyo itakuwa kichwani mwao itawafanya waishie kuokota makopo bila hata senti mfukoni kama hawaongoki na kutubu na kuacha huo uovu. Kuna wanaokosesha watu haki zao, maskini, wajane, yatima kwa kuchukua rushwa na kupinda haki. Nawaombea waongoke kabla hiyo rushwa haijawatokea puani. Mafisadi wanachota mabilioni ya fedha wakati kuna watu wanashindia mlo mmoja kwa siku na kwa shida, watoto hawaendi shule kwa kukosa ada na vifaa, magonjwa yanauwa watu kwa kukosa dawa. Fisadi unahitaji shilingi ngapi kuishi vizuri, manyumba mangapi ulale vizuri, magari mangapi upate usafiri, viwanja vingapi ujenge nyumba? Je pesa hizo zote unazoiba bila huruma za nini? Pole hutanunua furaha au amani, ingawa utakuwa na majumba mengi ya fahari utashindwa kulala kwa amani hata katika kachumba kamoja, viwanja vyako vilivyojaa kila mahali hutajenga makazi ya upendo, magari yako ya fahari hayatakufikisha popote, biashara yako ya bandia itakupa kichaa. Tubu haraka au utaukosa ufalme wa milele. Kuwa kama Zakeo rudisha kila kitu ulichoiba na faida yake na inayobaki wasaidie maskini na wenye shida. Tumwombe Mungu atuepushe na mafisadi, ni balaa kubwa sana. Tuwe na viongozi wasio kuwa kama Pilato anayeogopa kusema ukweli, wenye kukataa shinikizo la ubaya. Waweze kuwakabili hawa mafisadi na kutokomeza ufisadi ili kila mtu ajue na kuelewa kwamba ufisadi hauna tija, haulipi hapo tu nipo utakoma. Wajue kwamba ukiwa fisadi ole wako utafute shimo la kujificha, hapo utakoma. Tusiwe na viongozi kama wakuu wa Wayahudi ambao shida yao ni woga wa kupoteza kula yao, madaraka, cheo na kwa kulindai masilai yao hayo wako tayari kumwua Yesu ili waendelee kukandamiza. Lakini tumshukuru Mungu kuna wengi walio na huzuni kwa ajili ya Yesu, ukianzia na mama yake Maria na wanawake waliomsindikiza, alikutana na wanawake njiani wakimlilia, kuna Simoni wa Kirene aliyemsaidia msalaba na wengine wengi waliokuwa na uchungu. Nasi tumwombe Mungu tuwe kama hao wanaoungana na mateso ya Bwana; wanaowajali maskini, wajane, wasio na sauti, yatima na wanyonge. Kuna kati yetu wanaotetea haki hata kama nikuweka maisha yao rehani. Kuna wanaolia kama Yohana Mbatizaji nyikani wakisema tubuni. Mungu awadumishe na kuwapa ujasiri. Katika ibada hii tutakuwa na maombi mbali mbali kwa ajili ya shida na matukio. Tutaliombea kanisa, viongozi wake waamini na wakatekumeni; tutawaombea wakristu wengine, wayahudi, wa dini za jadi, wasioamini nk. Naomba nawe uungane nami uongezee maombi yako kwa sababu huu ndio wakati maalum Kristo anapokufa kwa ajili yako na yangu. Kati ya maombi nitakayoyatoa rasmi kwa namna ya pekee tutawaombea viongozi wetu hasa wa hapa Tanzania tuwaombee maalumu, wawe imara katika kusimamia haki bila kuongopa mtu au kupendelea mtu ili taifa liweze kuwa salama. Tumwombee Rais wetu, mawaziri, wabunge, mahakama, viongozi wa serikali, vyama na taasisi. Tuwaombee wawe kama mfalme Sulemani alipopewa na Mungu fursa ya kuomba anachotaka aliomba busara na hekima ya kuamua kilicho haki na kupambanua kati ya chema na kibaya. Nasi leo hatuwaombei utajiri wa haraka haraka, au vyeo vikubwa, hatuwaombei fahari na raha bali kama mfalme Sulemani tuwaombee hekima na busara ya kutofautisha kati ya ngano na pumba, ya chema na kibaya, haki na uonevu, kati ya utumishi na wizi, huduma na rushwa, uongozi na ubabe, ushirikishaji na uswaiba, uchapakazi na uvivu, ushauri na ushabiki, ujasiliamali na ujambazi, uwekezaji na ufisadi, utawala bora na umangimeza. Wajue kwamba mambo ya dunia kama utajiri, umaarufu na ukubwa ni kama kivuli, ukikimbiza na kufukazana nacho hukipati kila mara kinakuacha lakini ukikipuuzia na kufanya mambo ya haki, ya heshima na utauwa, kinakufuata kila mahali uendapo. Mungu wape fadhila ya utu, uwajibikaji na uaminifu. Mama tazama mwanao Yesu anamwambia Mama yake Maria ampokee Yohana kama mwanae, na vile vile anamwambia Yohana tazama mama yako. Kwa maneno hayo ametukabidhi sote kwa mama yetu Maria. Yule Maria aliyepokea maiti ya mwanae toka msalabani ikiwa haina uhai na uso hautambuliki tena. Huyu ndiye mama yetu anayetembea na sisi katika shida zote kumwendea Mwane asemaye njooni kwangu nyote msumbukao na kulemewa na mizigo mimi nitawapumzisha kwa sababu nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi. Tumbusu Kristu aliyesulubiwa msalabani na kufa kwa ajili yetu, tubusu msalaba wake kwa upendo na toba tukimwahidi kuwa waaminifu kwake. Mzigo mkubwa anaubeba yeye sisi anatuachia ule mwepesi. Ni kwake tu kuna uzima na wokovu. Nawatakia kumaliza vcema juma takatifu na kusheherekea vizuri siku ya pasaka tukiwa tumefufuka naye. AMINA

No comments:

Google+ Followers

There was an error in this gadget
There was an error in this gadget

Arts n' Photo sildes

"SILENT VOICES" PHOTO EXHIBITION

Future Stars!

Some of published work

RIGHT TO BE RICH

RIGHT TO BE RICH
The ownership of money and property comes as a result of doing things in a certain way, and those who do things in this certain way — whether on purpose or accidentally — get rich, while those who do not do things in this certain way — no matter how hard they work or how able they are — remain poor. WDW Do things in RIGHT way now, but how? Call: +255716927070/+255784475576

Popular Posts

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...