Pages

September 29, 2011

Nani kuwalipa Dowans Bilions 111?



Nani kuwalipa Dowans Bilions 111

Je ni nani atalipa Mabilioni hayo, kati ya Serikali na Tanesco, baada ya Mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali pingamizi la kutaka kuzuia kusajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania kwa tuzo ya Billion 94 (na riba ya 7.5% toka Nov 2010) dhidi ya Dowans Tanzania iliyotolewa na Mahakama ya kimataifa ya usuluishi ya kibiashara ICC?


Wengi tulitarajia hukumu hii, sababu ni nyingi, moja wapo ni ukweli kuwa Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu walishasema tuzo hii haipingiki, hivo walienda kupambana wakiwa wameshashindwa (psychologically), hivyo kilichokuwa kinafanyika ni ucheleweshaji tu.


Mjadala sasa ni nani anastahili kulipa tuzo hii au Mibilioni hii? kati ya Serikali kupitia wizara ya nishati na madini na Tanesco.


Akitoa maoni yake juu ya hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe alisema hukumu hiyo ni matokeo ya siasa mbovu.“Tumeingiza nchi hasara kwa sababu ya uongozi dhaifu na siasa za makundi ya CCM,” alisema Zitto na kuongeza:
“Hata hivyo, Tanesco hawawezi kulipa fidia hiyo kwani walilazimishwa kuingia mkataba na hata kuvunja mkataba huo.”


Alisema kamati yake imeshaagiza deni hilo lisitokee katika hesabu za Tanesco na badala yake lilipwe na Serikali.


“Hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amegoma kusaini hesabu za Tanesco za mwaka 2010 mpaka Serikali ikubali kubeba mzigo huo,” alisema Zitto.


Ikiwa hivyo ndivyo, kwamba Tanesco walilazimishwa kuingia mkataba ule na pia kulazimishwa kuuvunja, je ni nani aliyekuwa akiotoa ushauri huu wa kisheria, wa kulazimisha kuingia mkataba na baadaye baada ya kuona mazingira ni mwafaka kwake au kwao kuilazimisha Tanesco kuvunja mkataba?


Je ni mwanasheria mkuu wa serikali, ni waziri wa wizari husika au ni nguvu fulani juu ya wote hao? Anyway hilo lahitaji mjadala wake, lakini kwa sasa tuulizane, ni nani alipe deni hili? Kama ni wizara ambayo sote twajua kuwa bajeti yake ilipita kwa mbinde baada ya kukataliwa mara ya kwanza, je itakuwa na fungu la kulipa deni hili?



Ikumbuke kwamba tuzo hii ina riba ya asilimia 7.5, hivyo hakuna hasara yoyote kwa Dowans bali serikali na taifa kwa ujumla, hata hivyo ni nani mmiliki halali wa Dowans anayestahili kulipwa mabilioni yote hayo? Je ni huyu Mheshimiwa wetu aliyetajwa mara kadhaa ktk hukumu ya ICC au ni yule mwarabu aliyekuja na kusema yeye ndio mwenyewe na kuacha maswali mengi kuliko majibu?



Kama ni yule siwezi kumsemea, hatujui watanzania na wala hajui matatizo yetu, wala hajui kuwa kuna watu wagonjwa wanakufa kila siku kwa sababu hospitali hazina dawa na yeye hana pesa ya kununulia wanakufa, au kwamba kuna shule tena za sekondari hazina madawati wala vitabu vya kiada achilia mbali maabara na uhaba wa wali, hajui kuwa kuna migomo inayoashiria kuanza ata kabla muhula wa masomo haujaanza wa vyuo vya elimu ya juu kwa sababu tu ya wanafunzi wengi wanaostahili kukosa mkopo, siwezi kumsemea, kwa hayajui haya.



Lakini kama ni huyu mheshimiwa wetu, ambaye “tunadhani” (pengine sivyo) anaijua Bongo yetu kindakindaki, anajuia changamoto zetu zoote, za elimu, afya, miundombinu, uchumi nk. Huyu naweza kidogo si kumsemea bali kumuomba awe na huruma kidogo na watanzania “wenzake” (sina hakika), awe na imani ata kama ni siasa uchwara ndio zimemuondoa katika kiti kile afahamu kuwa kwa Mungu hakuna kiti kile, hakuna uheshimiwa, hakuna utajiri wala utapewa nafasi ya mbele kwa sababu ulishinda kesi ICC.



Huyu namuomba avae viatu vya wale kina mama wajawazito wanaokufa kila siku kwa matatizo ya kukosa huduma bora wakati wa kujifungua, au ajiweke katika nafasi ya watoto hawa ambao madawati kwao ni msamiati usiokuwepo kwenye kamusi yao, pengine avae japo kihisia uhusika wa kijana yule aliyeuwawa kwa deni la sh 500 tu!, na labda avae viatu vya ndugu zetu Wazanzibar na madhira yaliyowakuta hivi karibuni kwa kukosa tu usafiri wa uhakika, roho nyingi zimepotea. 



Mifano ni mingi sana mingine anayo yeye mwenyewe, amewai pengine kukutana nayo, ya jinsi gani watanzania wana changamoto ambazo zinahitaji pesa nyingi sana kukabilina nazo na si kutoa katika kile kiduchu walichobahatika kukipata, pesa haiwezi kutufikisha mbinguni, ata kama tutajikusanyia pesa na mali nyingi kiasi gani hatuwezi kuondoka nazo, tutaziacha hapa hapa duniani.



Yawezekana tukasema kuwa twawekeza kwa ajiri ya watoto wetu, lakini je kwa mali ya dhuruma twaweka msingi gani kwa waridhi wetu? labda salamu za Nabii T. B Joshua za mwaka mpya zinaweza kumpa ujumbe.  

Chonde chonde Mheshimiwa kuwa na moyo wa imani kwa watanzania wenzio, samehe tuzo hii au itoe kwa idara au asasi maalumu, labda iboreshe elimu, afya au ata miundombinu, ata kama ni kwa jimbo la Igunga, hii itakupa heshima kubwa mbele ya jamii na dunia kwa ujumla kuliko yale yatakayo tokea iwapo serikali italazimika kukopa ama kuchukua fungu la fedha toka kwenye bajeti ambayo ni finyu kukulipa wewe. 

Huu ni mtizamo wangu, binadamu tumeumbwa tofauti, si ajabu wewe au mtu mwingine asikubaliane nao. 

Bernard Rwebangira,
Bongo Pix Blog. 

No comments:

Post a Comment