Pages

September 28, 2011

Kampeni Igunga zahamia angani, CHADEMA waanza, CCM na CUF kufuata leo.



WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilitikisa anga la Igunga baada ya kuanza kutumia helikopta kufanya kampeni zake, zile mbili za wapinzani wao, CCM zikishindwa kuwasili jimboni humo na kubaki Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kutokana na sababu za kiufundi.Wakati Chadema ikipasua anga na mbili za CCM zikibaki KIA, helikopta ya Chama cha Wananchi (CUF) nayo imeshindwa kutua Igunga jana na sasa inatarajiwa hapa leo.

 Helikopta ya Chadema ilianza kuonekana katika anga la Igunga saa 10:40 jioni ikiwa na maandishi makubwa ya chama hicho na rangi ya bluu.Ujio wa helikopta hiyo ulivuta kwa muda idadi kubwa ya wananchi waliokuwa kwenye Viwanja vya Sabasaba wakisubiri ujio wa helikopta mbili za CCM, ambazo awali, ilielezwa kuwa zingewasili saa 8:00 mchana.

 Baadaye ilielezwa kwamba helikopta hizo za CCM zingetua Igunga saa 11:30 jioni zikiwa na makada wa chama hicho akiwamo Katibu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba.

 Hata hivyo, ilipofika saa 12:00 jioni, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde akitumia gari la matangazo la Bendi ya muziki ya ToT Plus alitangaza kwamba helikopta hizo zisingeweza kutua Igunga kutokana na sababu za kiufundi.

Alisema zilichelewa kupata vibali kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam na kwamba baada ya kutua KIA ilishauriwa kuwa ni vyema zilale hapo.

 Alisema kama helikopta hizo zingeondoka KIA jana jioni na kufika hapa usiku wakati tayari kungekuwa na giza kitu ambacho kisingekuwa kizuri kiusalama. Alisema helikopta hizo sasa zitawasili leo saa 4:00 asubuhi.

 Matumizi hayo ya helikopta yanawafanya wananchi wa Igunga kushuhudia kampeni nzito na za aina yake tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa vyama hivyo mwaka 1994 na Rostam Aziz kushinda.Jimbo hilo lenye wapiga kura 170,000 katika vijiji 96, halijawahi kushuhudia kampeni nzito kiasi hicho zinazohanikizwa na magari yenye vifaa vya kisasa vya muziki.
 

Habari kutoka ndani ya CCM, zinaeleza kuwa katika kujihakikishia kura katika kipindi hiki cha lala salama, chama hicho kitawatumia makada wake, Makamba na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli wanaoelezwa kuwa na ushawishi mkubwa.

 Kulingana na vyanzo mbalimbali vya habari, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni za CCM anatarajiwa kurudi tena hapa keshokutwa.Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye aliwasili hapa jana kuongeza nguvu kwa viongozi wa chama hicho ambacho idadi kubwa ya wabunge wake wameweka kambi hapa.
soma zaidi hapa 

Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment