Pages

September 26, 2011

CCM WATWANGA MWANDISHI WA HABARI


MAKADA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walio katika timu ya kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Igunga, wameendelea kuandamwa na kashfa za matukio ya vurugu baada ya walinzi wa chama hicho (mabaunsa) kumpiga mwandishi wa habari wa gazeti la Dira ya Mtanzania, Mussa Mukama, na kunyang’anywa vifaa vya kazi na fedha. 

Akizungumzia tukio hilo, Mukama alisema alikwenda katika Hoteli ya Peak saa moja jioni walikofikia viongozi wa CCM kufanya mahojiano na Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya, kuhusu tukio la juzi la kurushiana risasi na kusababisha gari lake kuvunjwa vioo.

 Mukama alisema akiwa ameambatana na mwandishi wa kujitegemea, George Maziku, alizuiwa na walinzi wa CCM kuingia ndani, hali iliyowalazimu kuwasiliana na Bulaya kwa njia ya simu. 

“Tulimpigia simu Bulaya, ambaye alikuja langoni na kuwataka walinzi waturuhusu kuingia ndani,” alisema mwandishi huyo.

 Hata hivyo, alisema, ilipofika saa 3 usiku, waliagana na Bulaya lakini walipofika langoni yeye aliitwa na mlinzi mmoja ambaye baada ya kumfikia, alishangaa akimkaba na baadaye watu wengine wakajitokeza na kumshambulia kwa mateke, ngumi na makofi na kumnyang’anya fedha sh 423,000, modem na flash.

 Aliongeza watu hao wapatao wanane waliokuwa na sare za CCM na wengine nguo za kawaida waliendelea kumshambulia hadi walipozuiwa na mtu mmoja aliyetoka ndani ya hoteli hiyo. 

“Jamaa walipokuwa wakinipiga walitaka kuninyang’anya laptop yangu; nilipojaribu kumpigia simu Bulaya kumjulisha kilichonipata langoni, simu yake iliita bila kupokelewa,” alisema. 

Aliongeza kuwa baada ya hapo alipata msaada kutoka kwa mwandishi mwenzake, Maziku, aliyekwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi Igunga na kupewa PF3 ya kutibiwa hospitali ya wilaya. 

Alisema polisi walimpa RB namba 1673/2011 na kisha alipata matibabu na kuruhusiwa. Maziku alisema wakati wanatoka ndani ya hoteli alikuwa ametangulia mbele na Mukama akiwa nyuma; na mwenzake alipoitwa na mlinzi hakuwa na wasiwasi, lakini ghafla aliona wakimshambulia na alishindwa kutokana na wingi wa mabaunsa. 

Akizungumzia tukio hilo, Bulaya alisema amesikitishwa na kitendo ambacho ametendewa mwandishi huyo. 

Alisema kuwa baada ya mahojiano hayo aliingia katika kikao ambacho aliamua kuondoa mlio kwenye simu yake, hivyo hakusikia alipopigiwa na Mukama kuomba msaada.

Source: Tanzania Daima.
Ndipo siasa za Bongo zilipofikia sasa hivi. Hii ni hatari hatua za dharura zisipochukuliwa.  

No comments:

Post a Comment