Pages

October 9, 2011

CHADEMA WISHES JK HAPPY BIRTHDAY

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimlisha kipande cha keki mumewe, Rais Jakaya Kikwete wakati wa hafla ya kutimiza miaka 61 ya kuzaliwa kwake iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam. Anayeshuhudia ni mwanawe, Ridhwani Kikwete na mkewe pamoja na mtoto wao, Aziza. 


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimempa masharti magumu Rais Jakaya Kikwete kutokana na hukumu ya Mahakama Kuu kutaka Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) lilipe tuzo ya sh bilioni 94 kwa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans.

 CHADEMA imemtaka Rais Kikwete kuwachukulia hatua wote waliosababisha taifa liingie katika misukosuko hiyo ya mikataba ya umeme inayoliingizia hasara.

 Zaidi ya hayo, inataka watu hao ndio walipe tuzo ya Dowans, badala ya kulipa kwa kutumia pesa za walipa kodi kupitia TANESCO. 

Kauli hiyo ya CHADEMA ilitolewa jana na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, akisema Rais Kikwete anapaswa asome alama za nyakati sasa, kama anataka kuepusha maafa kwa taifa.

 Alisema walioandaa na kusaini mkataba huo ni viongozi wa serikali iliyo madarakani, na kwamba lazima wachukuliwe hatua kali.

 “Tunaipa serikali mwezi mmoja itoe kauli na kuchukua hatua… iwapo serikali haitachukua hatua kuanzia sakata la Richmond na Dowans, na bado ikaendelea na msimamo bila kutoa kauli ya kutolipa tuzo hiyo ambayo kwa sasa imefikia sh bilioni 111, tutaungana na wanaharakati kufanya maandamano nchi nzima kupinga malipo haya,” alisema Mnyika na kuongeza:

 “Hatuwezi kuona fedha za walipakodi zinachezewa kwa mkataba huu wa kifisadi… CHADEMA tunahitaji waliohusika wakamatwe na mali zao zifilisiwe ili kulipa deni hilo sambamba na kufikishwa mahakamani kwa uhujumu uchumi.”

 Mnyika alisema kutokana na mkataba huo ulioingiwa kwa uzembe na watu wachache kwa masilahi yao binafsi, CHADEMA itaendelea kuratibu maandamano ambayo walikuwa wameyaanza nchi nzima ya kupinga malipo hayo.

 Waziri huyo Kivuli, alisema inashangaza kuona serikali inajiita sikivu lakini imeshindwa kulipa madeni sugu ya muda mrefu, kama ya wazee wastafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977, na deni la walimu linalofikia sh bilioni 29, halafu inakimbilia kulipa deni la mabilioni kwa Dowans.

 Hata hivyo alisema hadi sasa wanafanya mawasiliano na vyanzo vya habari kutoka vilivyopo ndani ya serikali ili kuweza kujua azima ya serikali kuhusu sakata hili mara baada ya hukumu ya Mahakama Kuu kutolewa.

 Alisema Dowans haistahili kulipwa kwa sababu mkataba wake una uhusiano na Kampuni feki ya Richmond, ambayo wabunge wa CCM, wakiongozwa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, na kundi la waliojiita wapambanaji wa ufisadi ndani ya CCM, walitumia wingi wao bungeni kuzima sakata la Richmond, baada ya kuwa wameshinikiza kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri kadhaa mwaka 2008.

 Septemba 28, mwaka huu Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ilisajili tuzo ya sh bilioni 94 ya Dowans ambayo TANESCO na wanaharakati walikuwa wakipinga isisajiliwe.

 Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Emilian Mushi, akisema tuzo hiyo imesajiliwa kutokana na makubaliano ambayo TANESCO iliingia na Dowans katika mkataba wa pande hizo mbili.

 Mojawapo ya makubaliano hayo ilikuwa kwamba uamuzi utakaotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) ndio utakuwa wa mwisho.

 Makubaliano mengine ni kwamba pamoja na ICC kuwa na uamuzi wa mwisho, hakutakuwa na ukataji wa rufaa kama upande mmoja utashindwa.

 Pamoja na hilo, Dowans na TANESCO walikubaliana kuwa mmoja kati yao atakayeshinda kesi ya tuzo hiyo, atalazimika kumlipa mwenzake mara moja.

 Kutokana na makubaliano hayo, Jaji Mushi, alisema Mahakama ya ICC ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo, hivyo Mahakama Kuu haina mamlaka ya kutoa maamuzi mengine.

 Hata hivyo, Jaji Mushi alisema upande ulioshindwa una haki ya kuiomba mahakama iweke tuzo hiyo kando kama wameona kulikuwa na makosa ya kisheria.

CHONDE CHONDE ROSTAM  SOMA ARAMA ZA NYAKATI. 

No comments:

Post a Comment