Pages

September 20, 2011

Vimbwanga Igunga - Mbunge CCM: Tukishindwa nakunywa sumu



KAMPENI za uchaguzi mdogo katika jimbo la Igunga, zimezidi kupamba moto baada ya Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), kujiapiza mbele ya wananchi kuwa atakunywa sumu iwapo chama hicho kitashindwa kwenye uchaguzi huo.

 Akizungumza na wanakijiji wa Ugaka kwenye kata ya Nkinga wilayani hapa wakati akimwombea kura mgombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu, Lusinde alisema kutokana na mwenendo mzuri wa kampeni za CCM na jinsi wanavyowafikia wananchi, haoni sababu za kushindwa kwenye uchaguzi huo.

 “Hapa nimewaona waandishi wa gazeti la Mbowe (Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA); nataka mkaandike kwa namna ambavyo tumezunguka, CCM tukishindwa nakunywa sumu,” alisema na kuongeza:

 “Nataka tuwaambie, tutawapiga bao la mbali kabisa na huyo Dk. Slaa sisi tunammudu ndiyo maana tukamwambia Mzee Kikwete, endelea kuongoza nchi atuache vijana tumkabe koo maana yule mzee ni mnafiki mkubwa,” alisema Lusinde.

 “Kale kazee kagonjwa kale, ndiyo maana nimekuja kuwaambia inawezekana viongozi wa CHADEMA wanavuta bangi, zile bangi zile, haiwezekani unatembea nchi nzima unahamasisha vurugu, unatangaza vita,” alisema Lusinde Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.

 Kwa upande wake mratibu wa kampeni hizo, Mwigulu Mchemba, aliwataka wananchi hao kumchagua Dk. Kafumu na kusema wanasiasa wa upinzani wanasema tangu uhuru serikali ya CCM haijafanya kitu kabisa, Igunga haijapata maendeleo wakati si kweli.
 

“Wenzetu wanapandikiza chuki kwa vijana wa vyuo vikuu nao wanakubali kupotoshwa na wanasema serikali ya CCM haijafanya kitu si kweli. Kwanza idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu imeongezeka halafu wanasema Rais huyu hajafanya kitu, kama si kulaaniwa ni nini?” alihoji.

 Alisema wapinzani wanatumia umaskini wa wananchi kama mtaji wa kisiasa, wamelalamikia kupandishwa kwa bei ya pamba ili watu wakasirike na kutoichagua CCM.

 “Wacha niwaambie wakati wa ukame serikali ya CCM iligawa chakula jimbo lilipokuwa wazi wakasema tusigawe chakula eti hiyo ni rushwa sasa tusipogawa chakula mtatuchagua? Hivi njaa ina likizo? Kwa nini serikali ipeleke chakula mpaka Somalia lakini Igunga ibaki na njaa hivi mtapiga kura mkiwa na njaa?” alihoji Mwigulu.

Source: Tanzania Daima.

No comments:

Post a Comment