Pages

September 20, 2011

Nani wanahujumu Sukari???


 Kampuni Kilombero yashangaa uhaba wa sukari


KAMPUNI ya Sukari Kilombero imeshangazwa na nchi kukumbwa na uhaba wa sukari, ikisema kuna hujuma kwenye usafirishaji nje ya nchi bidhaa hiyo, kwani kwa miezi mitatu Tanzania imekuwa ikilisha sukari Kenya.

 Imesema yenyewe huzalisha sukari ya kutosha kwa wastani wa tani 500 kwa siku na kuwapa mawakala wake, lakini kuna watu wanauza nje ya nchi ambako sukari ina bei maradufu ya bei ya ndani ya nchi hali hiyo inachangia uhaba huo.

 Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni hiyo, Bashir Harun, alimweleza hayo Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe alipotembelea kampuni hiyo Dar es Salaam kufahamu hali ya uzalishaji na usambazaji wa sukari.

 Harun katika kuthibitisha hujuma katika usambazaji wa sukari, alisema wapo wafanyabiashara wanaoingiza fedha katika akaunti ya kampuni hiyo kwa lazima wakitaka sukari.

 Alisema kitendo hicho kiliwalazimu kuandikia benki zote barua kuzizuia kupokea fedha ili kuhakikisha mikoa yote inapata sukari kupitia mawakala wake.

 Alisema muda kama huu, kiwanda chake huwa na sukari ya ziada, lakini mwaka huu hakina kutokana na kuwa yote inauzwa, akitolea mfano wa mwaka jana ambapo mwezi kama huu walikuwa na ziada ya tani 18,500.

 “Kinachotakiwa Waziri ni kufanya kazi kwa ushirikiano na kuanzia leo nitakupa kiasi kilichozalishwa na kila wakala amechukua kiasi gani cha sukari ili kumfuatilia anaipeleka wapi na anaigawa vipi,” alisema na kuahidi kumpa Waziri orodha ya wasambazaji na mawasiliano yao.

 Aliwataja baadhi ya wasambazaji anaowapa sukari kwa kila mkoa kuwa ni Iringa (Kaundama Store), Morogoro (MA Traders,Thabit Islam, Alnaeem na Mohamed Enterprises).

 Wengine ni Mtwara (MA Abdurazack), Mwanza (VA Shah), Mbeya (Tugimbane), Shinyanga (Alneeem na Mohamed Enterprises) na Dodoma (Mnary na Anthony Alex) na Dar es Salaam (RTC, Mohamed Enterprises na wengineo).

 Harun alisema huwauzia kilo 50 za sukari mawakala hao hadi Dar es Salaam kwa kati ya Sh 82,600 na Sh 85,000 huku bei ya kiwanda ikiwa Sh 80,004.

 Waziri Maghembe alisema kuanzia leo watafuatilia magari yote kutoka kiwandani mpaka yanakokwenda kwa kutumia watu maalumu na atakayegundulika sukari aliyotoa kiwandani haijawafikia wananchi, atafutiwa leseni.

 “Baada ya kuwafutia leseni nitawapa taarifa viwanda vyote kutomwuzia sukari tena kwani haiwezekani kuzalisha sukari kwa ajili ya nchi jirani huku wakisafirisha bila leseni, kwani Serikali haijapata kutoa leseni ya kuuza sukari nje,” alisema Maghembe.

 Alisema ni lazima kufahamu sukari inakwenda wapi na nani anaipeleka, kwani Serikali haitaki sukari ya nje kuingia nchini, ili kulinda viwanda visife, kwani hali hiyo itakuwa haiwatendei haki Watanzania.

 Alisema kwa msambazaji ye yote atakayepakia mzigo na akashindwa kusema anakoupeleka, sukari hiyo itachukuliwa na Serikali lengo likiwa ni kuifikisha kwa mlaji.

 Aliwataka wananchi kupiga simu namba 0754-387928 kutoa taarifa za watu wanaohodhi sukari kwenye maghala au kuuza nje ya nchi na watoa taarifa watapewa zawadi.

source: Habari Leo,
Picha na Leonald Magomba

No comments:

Post a Comment