Pages

September 9, 2011

Mwisho wa Tanesco umekaribia???


Serikali yaridhia sekta binafsi kwenye umeme


KATIKA  kukabiliana na tatizo la ukosefu wa umeme wa uhakika nchini, serikali imekusudia kufanyia marekebisho sheria ili kuwaruhusu watu na taasisi binafsi kuzalisha na kuzambaza umeme bila kuupitishia Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO).

 Hayo yalisemwa jana jijini Arusha na Waziri wa Fedha na Uchumi , Mustafa Mkulo, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Bilali, kufungua mkutano wa 20 wa magavana wa nchi za Afrika, unaojadili tatizo la ajira kwa vijana na matumizi ya fedha za maendeleo zinazotolewa na wafadhili.

 Alisema kuwa sheria hiyo itapelekwa bungeni kwenye kikao cha Novemba ambapo kama wabunge wataridhia mabadiliko hayo, yatawezesha  umeme kusambazwa maeneo mengi hasa ya vijijini  jambo litakalosaidia kupunguza wimbi la vijana kukimbilia mijini kutafuta ajira kwani wataweza kuendesha shughuli za kujiajiri.

 “Kuna taasisi na kampuni ambazo zinazalisha umeme wao na mwingine mwingi wa ziada  unabaki lakini wanashindwa kuusambaza hata kwa majirani zao kutokana na sheria ya sasa hairuhusu  lakini tukibadilisha sheria ya sasa, wengine watajitokeza kuzalisha na kusambaza kwa wananchi hivyo kupunguza tatizo, ” alisema Waziri Mkulo.

 Alisema kuwa tatizo la ajira kwa vijana lililopo barani Afrika na hapa nchini linaweza kutatuliwa endapo kutakuwa na mkakati wa pamoja kuhakikisha kuwa vijana hao wanapatiwa elimu ya kuwawezesha kujiajiri mara baada ya kumaliza masomo, badala ya kusubiri kuajiriwa, hivyo alivitaka vyuo vikuu kuhakikisha vinabadili mtazamo na kutoa elimu itakayowawezesha vijana kujiajiri  mara baada ya kuhitimu mafunzo.
“Kwenye bajeti ya mwaka huu tumeitengea fedha nyingi  Wizara ya Elimu na Mafunzo ili iweze kuboresha vyuo vya ufundi  stadi (VETA) pamoja na  SIDO (Shirika la Viwanda Vidogo) ili kutoa mafunzo ya ufundi  kwa vijana yatakayowawezesha kujiajiri,” alisema Waziri Mkulo.

 Katika kuwahakikishia soko la bidhaa zinazozalishwa na vijana kupitia ufundi, alisema kuwa serikali ilishapiga marufuku  watendaji wake kuagiza  samani kutoka nje ya nchi na badala yake wanunue zile zinazotengenezwa hapa nchini lakini wanunue zilizo na ubora unaokubalika.

 Aidha aliwataka wananchi  wenye uwezo kujitokeza kuliendesha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa ubia na serikali katika kutekeleza sera ya ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP)  ili kuongeza ajira  hasa kwa vijana, huku akisisitiza kuwa jina halitabadilishwa.



Uenda hii ikawa faraja kwa walio wengi. tusubiri tuone. 

No comments:

Post a Comment