Pages

September 12, 2011

Mv Spice Islander - Simulizi ya Baharia

  • Nahodha, Mabaharia 11 hawajulikani walipo,
  • Mamia bado hawajulikani walipo,
  • Wazamiaji 12 toka Afrika kusini wawasili na vifaa vya kisasa kusaidia uokoaji.
  • Leo ni siku ya mapumziko Visiwani
  • Dua maalumu yasomwa katika viwanja vya Maisara


Baharia Rashid Said Rashid wa meli ya Mv. Spice Islander, iliyozama na kuua takribani watu 240 huku wengine 619 wakinusurika visiwani Zanzibar juzi, amesema waligawa maboya ya kujiokoa kwa abiria na kuwavalisha watoto kisha kuwaondoa melini kupitia madirishani kabla ya kuzama.
Akizungumza na NIPASHE akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, jana, alisema kabla ya meli hiyo iliyokuwa na mabaharia 12 kuzama majira ya saa 7:00 usiku wa Ijumaa iliyopita eneo la Nungwi, waliomba msaada kwa meli nyingine iliyokuwa inapita lakini hawakufanikiwa.
Said ambaye ni mkazi wa Shangani, alisema baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya kabla ya meli kupinduka, abiria walimtaka nahodha atoe taarifa kwao kama meli inazama na alifanya hivyo.
“Tulijaribu kufanya kila jitihada ili kuokoa hali hiyo, lakini tulishindwa na tukaamua tuiache meli na kuanza kutoka, hapo tena kila mmoja alikwenda kwa upande wake,” alisema.
Hata hivyo, alisema hafahamu kama mabaharia wenzake na nahodha wapo salama au wamekufa kwa sababu mara ya mwisho aliwaona kabla ya chombo kupinduka na kuzama.
“Kwa kweli siwezi kusema kama ni uzembe au la umefanyika, lakini wakati inatokea hali hii tulipishana na meli ya MV Jitihada na kuwapa ishara ya kuzama, lakini hawakutusaidia,” alisema baharia huyo.
Alisimulia kuwa walichukua jitihada mbalimbali za kuwapa ishara, lakini hawakufanikiwa na hawezi kusema kama walidharau au hawakuwaelewa walichokuwa wakikitafuta kutoka kwao.
Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment