Pages

September 14, 2011

Miaka 5 ya Kublog


Miaka mitano iliyopita mwezi kama huu na tarehe kama Bongo Pix Blog ilizaliwa, post ya kwanza iliwekwa katika blog, hayakuwa maamuzi mepesi kuanza ku-blog katika mazingira ya wakati ule, wengi walikuwa wakiogopa hata kusikia, wakiichukulia kwa mtizamo hasi zaidi, bila shaka, ni hurka ya binadamu, kutokubali kwa urahisi jambo lolote jipya, hasa liwajialo tofauti na mazoea yao.

 Ilikuwa ngumu, wengi walikuwa wakituangalia kama watu wa ajabu kuwa na blog au globu (msemo wa gwiji la kublog nchini Ankal Michuzi), japo BPB ilianzishwa kwa kujifunza (self taught) lakini ilitokana na hamasa toka kwa blogaz kadhaa ambao walishatangulia katika fani kama Ndesanjo Macha, Isaa Michuzi na pia jukwaa la Jamii Forums wakati huo likijulikana kama Jambo Forums.

 Nikiangalia tulipo sasa sina shaka kukiri kuwa tumepiga hatua kubwa katika nyanja hii ya mitandao ya kijamii, hivi sasa watu wengi zaidi wameanzisha na kuendesha blogs, pia wapo wanaoendesha maisha yao kupitia blogs, yaani ni kama kina Murdoch au Mengi wadogo, wanamiliki vyombo vyao vya habari, mashirika makubwa na kampuni kadhaa zina viunganishi vya blogs katika wavuti zao, hii ni hatua kubwa.

 Jambo ambalo sikujua wakati ule naanza ku-blog ni kuwa huu ni kama ulevi vile, kila unapokaa wahisi kuandika ama kuhabarisha watu, kujuza ulimwengu juu ya yale yanayokuzunguka, wahabarisha watu ambao hamuonani, kuna wakati nilikuwa namaliza siku mbili au tatu sijapost kitu, najikuta napata comment au email, kuhoji kimya changu au kutaka kujua jambo fulani, ndipo wajua kumbe kuna watu wanakusoma mahali fulani. 

Katika kutimiza miaka mitano BPB ina mikakati kadhaa, mojawapo ni kufanya kile ambacho kilifanya kuanzishwa kwayo, UPASHANAJI HABARI KWA NJIA YA PICHA ZAIDI, hili lilikuwa lengo kuu la kuanzishwa kwake, picha ambazo mwisho wa siku zitaleta mabadiliko chanya katika jamii yetu, picha zina nguvu sana katika kuhabarisha na kuleta mjadala ambao mwisho wa siku ni mabadiliko chanya katika jamii.

 Toka kuvumbuliwa kwa fani hii ya picha dunia imeshuhudia mabadiliko mengi yaliyotokana na watu kuona picha na hivyo kuoji na kujadili na hatimaye kufikia makubaliano kuwa inabidi lifanyike jambo fulani kubadili hali husika, kwani picha si tu kwamba inaongea maneno 1000 bali inamfanya msomaji kuona uhalisia jambo kama yuko hapo kuliko maandishi ama sauti. Yapo mambo mengi sana katika jamii zetu (mazuri na mabaya, ya kuigwa na kukemewa) yanayo paswa kumulikwa hili yajulikane na kisha hatua fulani zichukuliwe, BPB katika miaka mitano ijayo itajikita katika jukumu hilo zaidi.

 
 Bongo Pix Blog

No comments:

Post a Comment