Pages

September 16, 2011

Igunga, Ngoma inogile

CHADEMA WAMKAMATA MKUU WA WILAYA YA IGUNGA. 

VURUGU zimezuka jana katika Kata ya Isakamaliwa, wilayani Igunga zikiwahusisha viongozi wa Chadema na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario.Katika sakata hilo, wanachama wa Chadema walimkamata Mkuu huyo wa Wilaya kwa tuhuma za kuendesha mkutano wa ndani na watendaji wa serikali za vijiji, wakati akijua kuwa kulikuwa na mkutano wa kampeni za chama hicho karibu na eneo hilo.
 
Msafara wa Chadema ulifika katika eneo la kampeni saa 8.00 mchana na kabla mkutano haujaanza, Meneja Kampeni wa chama hicho, Sylivester Kasulumbai, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mkuu wa wilaya ya igunga alikuwa akifanya kikao cha ndani katika eneo hilo kinyume na taratibu, hivyo wanakwenda kumshughulikia.
 
Kasulumbai ambaye ni Mbunge wa Maswa Mashariki akiwa na Mbunge wa Viti Maalum, Susan Kiwanga, baadhi ya wananchi na vijana wao, walifika katika ofisi ya Mtendaji wa Kata kulikokuwa kunafanyika mkutano huo na kuanza kuhoji aliko Mkuu huyo wa Wilaya.
 
Mmoja wa wananchi alimnyooshea kidole mama ambaye alikuwa amekaa mbele na kusema; “..yule ndiye Mkuu wa Wilaya”.Kundi hilo la vijana na viongozi wa Chadema, waliingia katika ukumbi huo na kumtoa nje mama huyo huku wakimtaka aeleze kwa nini anafanya vikao vya ndani katika Kata hiyo wakati anajua kuwa chama hicho kilikuwa na mkutano katika eneo hilo.
 
Kitendo hicho kilizua purukushani na kutokuelewana kati ya waliokuwa kwenye mkutano wa ndani na viongozi wa Chadema, jambo lililovuta umati mkubwa wa watu.
 
Maelezo ya DC
Baadhi ya vijana wa Chadema walikuwa wamewashikilia watu waliokuwa wakishiriki mkutano huo huku mama huyo akitolewa nje na kuketishwa kwenye kiti alitakiwa atoe maelezo kuhusu mkutano wake.
 
Baada ya kukaa kwenye kiti huku akionekana kuchanganyikiwa, alisema yeye ni Mkuu wa Wilaya ya Igunga, jina lake ni Fatma Kimario na kwamba, hakuwa na taarifa za mkutano wa kampeni za Chadema.
 
“Sina ratiba, iko katika ofisi za halmashauri, hivyo sikujua kama kuna mkutano hapa, hata hivyo watu walikuwepo niliwaruhusu waende mkutanoni na mimi nilikuwa naondoka sasa hivi,” alisema na kuongeza:
 
“Nilichokuwa nafanya ni mkutano wa viongozi wa serikali kwa ajili ya kuangalia hali ya mifugo inayoibwa sana, elimu kwa wote hasa watoto na ujenzi wa nyumba bora na masuala ya amani”.
 
Kimario aliwasihi wafuasi wa Chadema kusoma karatasi ya ajenda ili wafahamu kilichokuwa kikijadiliwa kwenye kikao hicho.
 
Karatasi aliyokuwa akiizungumzia Mkuu huyo wa Wilaya ilikuwa na ajenda tano za kikao hicho ambazo ni; Uhamishaji wa mifugo; Kuwa na choo chenye ubora na nyumba bora; Elimu;  Mipaka ya shule na ajenda ya mwisho ilikuwa Uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga.
 
Hata hivyo mbunge Kiwanga alimtaka mkuu huyo wa wilaya aeleze tangu lini kikao cha viongozi wa serikali kikahudhuriwa na wazee maarufu na mabalozi wa nyumba kumi, swali ambalo lilionekana kumchanganya mkuu huyo wa wilaya kwa kutoa majibu tata.

No comments:

Post a Comment