Hii inasikitisha sana, Familia nzima kuteketea na usijue waliko!!
Tulikuwa watu 36 wakubwa kwa watoto lakini walionusurika ni
wanne tu, 32 wote wamefariki dunia katika ajali hiyo na kati ya watu
waliofariki miili iliyoonekana ni saba waliobaki hawajaonekana mpaka sasa,”
alisema Ally na kuongeza:
“Ingawa mimi ni mzima lakini mpaka hivi sasa sijui pakuanzia
wala pa kutokea baada ya kutoka hospitali kwa sababu familia nzima imeteketea
katika ajali hiyo.”
Tulikusanyika wote tukasali
“Kwa kweli nilipoona hivyo nikajua sasa tumekwisha. Nikarudi
tena chini nikakuta maji yameshajaa ndani ya meli ndipo tukakusanyika wanandugu
wote tuliokuwa ndani ya meli pamoja na maharusi wetu tukaswali swala ya mwisho
na kuambizana kuwa kila mtu ajiokoe mwenyewe na Mungu akipenda tutakutana
popote pale iwe duniani ama peponi,” alisema Ally.
“Niliwakusanya watoto wote baada ya kuona wazazi wao
wamechanganyikiwa na ukizingatia kwamba hawana uzoefu na masuala ya maji
nikawapa godoro na kuwaambia kwamba walishikilie kwani ndilo itakalowaokoa.”
“Baada ya kuwapa watoto godoro, nikarudi kuwatafuta ndugu
wengine lakini sikufanikiwa kuwaona tena ndipo nilipoamua kurudi juu kutafuta
jaketi nikapata moja nikalivaa kisha nikarudi nilipowaacha watoto na kuungana
nao. Wakati huo maji yalikuwa yameshajaa ndani ya meli."
“Kidogo nikaokota mbao ambayo baadaye ilinisaidia kuvunjia
moja ya dirisha la meli hiyo kwani wakati huo hata mlango ulikuwa hauonekani
nikawapitisha watoto pamoja na mimi mwenyewe nikapita.”
“Nilipofika nje ya meli, nikakuta watu wengi wanaelea na
majaketi yao wengine wakiwa wameshafariki dunia, kwa sababu yale majaketi kama
hujui kuogelea hayawezi kukusaidia, isipokuwa ukifa huwezi kuzama badala yake
utakuwa ukielea juu ya maji. Kadri muda ulivyozidi niliona watoto wakizidiwa na
kuishiwa nguvu na mwishoni wote wakafariki dunia mbele yangu.”
Muda wote akisimulia, Ally alikuwa akibubujikwa machozi...
“Baada ya kuona ndugu zangu wote wameteketea, ndipo nilipoanza kujiokoa
mwenyewe na ilipofika saa 5:00 asubuhi, nikaona helikopta ikipita nikaanza
kupeperusha shati langu kila wakati mpaka waliponiona na kuja kuniokoa.”
“Walipofika wakashusha kamba nikajitahidi kujivisha kwa
shida kwani wakati huo wote hakuna hata kiungo changu kimoja kilichokuwa
kinafanya kazi mwili ulianza kuchanika kwa sababu ya chumvi na baridi kali.”
Miongoni mwa walionusika alikuwamo mtoto wa miaka sita akiwa
na dada yake mwenye umri wa miaka 12. Mama mdogo wa mtoto huyo, Mariam Hemedi
alisema Said anaendelea vizuri na dada yake amesharuhusiwa kutoka hospitali.
No comments:
Post a Comment