Pages

February 21, 2011

Mmiliki wa Dowans akataa kukutana na Ngeleja na kupigwa picha

WAKATI Mjadala wa Dowans ukibaki kwenye swali la nani mmiliki wake, raia wa Oman, Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi amejitokeza na kukiri kuimiliki kampuni hiyo inayoidai Tanzania mabilioni ya shilingi. Al Adawi alikutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini jana na kueleza ujio wake kuwa umelenga kukutana na Tanesco na kujadili suala la malipo ya Sh94 bilioni ambayo kampuni yake inaidai Tanzania.

Ujio wa Al Adawi umemaliza mjadala uliogubika umiliki wa Dowans na kuwachanganya Watanzania huku baadhi yao wakiamini kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz. Al Adawi ni mmoja wa watu ambao majina yao yako kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni nchini (Brela) waliojiandikisha kama wamiliki wa kampuni hiyo ya Dowans.

Watu wengine waliotajwa na Brela kuwa ni wamiliki wa Dowans Tanzania Ltd, ambao ni Dowans Holding S.A, Costa Rica na Portek Systems and Equipment (PTE) Ltd na uraia wao kwenye mabano ni Andrew James Tice na Guy Picard (Canada), Gopalakrishnan Balachandaran (India), Stanley Munai (Kenya) na Hon Sung Woo (Singapore).

Akizungumza katika mkutano huo huku akigoma kupigwa picha, Al Adawi alisema yuko tayari kuzungumza na Tanesco kuhusu fidia ya Sh94 bilioni (hakutaja kiasi), baada ya kuvunjwa kwa mkataba baina ya kampuni yake hiyo na Tanesco.

"Nimekuja kwa mambo mawili; moja ni kuondoa sintofahamu iliyopo hivi sasa kuhusu kampuni ya Dowans na kuangalia kama kuna uwezekano wa kuwapo suluhisho la kile kilichopo hivi sasa kuhusu Dowans," alisema Al Adawi. Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, ambaye ni Mwanajeshi aliyestaafu katika ngazi ya Brigedia Jenerali, Tanzania ni nchi inayovutia kibiashara na inayofuata sheria za uwekezaji.

Source: Mwananchi

1 comment: