Mhariri wa Daily News naye vipi?
NILIKWISHA kusema katika safu hii kwamba kipindi cha uchaguzi ni msimu wa vituko na vitimbwi, na kwamba watu wenye akili timamu wanaweza wakaziweka akili zao kando ili washiriki vyema katika shughuli za uchaguzi, kisha wazirejee akili zao na waendelee na shughuli zao za kila siku.
Hawa ni wengi, na tumewaona, tumewasikia na tutaendelea kuwaona na kuwasikia hadi mwishoni mwa Oktoba. Baada ya Oktoba watarudia hali zao za kawaida, na ukiwaangalia wakati huo hutoweza kuamini kwamba ndio wale wale uliowaona na kuwasikia mwezi Septemba.
Mhariri wa gazeti la kila siku Daily News naye kajiunga na kundi hilo kubwa, labda kwa sababu anachelea kuachwa nyuma katika mashindano ya kuweka akili kando kwa muda kama vile kuna manufaa fulani katika kufanya hivyo.
Mhariri huyo, inaelekea, alikerwa sana na taarifa iliyotoka katika gazeti moja linalotoka kila Jumanne (hakulitaja, na kwa siku yake ya kutoka si Raia Mwema!) iliyoarifu kwamba kura ya maoni iliyofanyika kupitia mtandao fulani iliashiria kwamba mgombea urais kupitia CHADEMA anakubalika kwa wale walioshiriki katika kutoa maoni hayo katika mtandao huo.
Taarifa hiyo ilimfanya mhariri huyo kuweka akili kando na kuingia kazini. Katika tahariri isiyo ya kawaida na iliyoanzia ukurasa wa mbele (kuonyesha kwamba hili lilikuwa jambo muhimu sana) mhariri huyo anataka watu wasilihusishe gazeti lake na taarifa ambayo ilitolewa na mtandao wa gazeti hilo hilo na mtandao mwingine wa watu binafsi.
Katika sehemu moja ya tahariri hiyo mhariri anasema: While noting the tabloid editors’ virtual confession that they cannot be believed without quoting the Daily News....
Hii ina maana kwamba mhariri wa gazeti hilo la aina ya tabloid (nitaeleza baadaye) anakiri kwamba ili anachosema kiaminike ni lazima alikariri gazeti la Daily News. Hii ni mantiki-pinda kwa mtu ye yote anayejifunza kufikiri.
Kama mtandao uliokaririwa ni wa gazeti hilo, na kama taarifa hizo kweli zilikuwamo katika mtandao huo, ni nini cha kumfanya mtu aamini kwamba kunukuu taarifa hizo ni kutafuta kuaminika kwa kutumia jina la gazeti hilo?
Mhariri anataka kujiliwaza kwa kusema kwamba gazeti linalochapishwa na Serikali ni chanzo cha kuaminika cha habari, lakini pasi na shaka nitakubaliana naye kwamba ikiwa gazeti hilo, au mtandao wake. litaweka kwenye tovuti taarifa inayoonyesha kwamba kundi fulani, dogo, lililoulizwa swali kuhusu nani anafaa kuwa rais na wengi wa kundi hilo dogo wakamtaja mgombea wa Upinzani, hiyo ni habari. Tatizo liko wapi?
Mhariri huyo ametumia neno confession hapo juu, na chini kidogo akatumia neno hilo tena kwa muundo wa they confess. Kuungama huku anakokuzungumzia mhariri ni kuungama kuhusu nini? Kama gazeti analolishutumu lilieleza kwamba Watanzania wanaotumia mtandao kupata habari ni wachache mno kiasi kwamba taarifa hizo zinatakiwa zipokelewe kwa hadhari inayopasa, kuna kosa gani hapo, na kuungama kunatoka wapi?
Asichosema mhariri wa Daily News ni kwamba mtandao wa gazeti lake on-line ulibeba taarifa hizo anazozilalamikia, ila anasema zilikaririwa out of context; yaani bila kuzingatia mazingira. Mimi nadhani kwamba mwandishi wa taarifa yo yote anapotoa tanbihi kwamba mchakato fulani uliwahusu watu wachache, na akatoa idadi yao, na kueleza kwamba taarifa hii isichukuliwe kama kigezo cha mambo yatakavyokuwa siku ya uchaguzi, huko ni kuzingatia mazingira.Lakini inavyoelekea mhariri wa Daily News ana hofu kubwa kuhusu uchaguzi huo, na hususan kuhusu kuwapo kwa taarifa kama hizo katika mtandao unaohusu gazeti lake. Haikosi kaulizwa maswali na tajiri wake kuhusu taarifa hiyo: Je, kuna mashabiki wa mgombea wa CHADEMA katika gazeti lako? Nani aliweka taarifa hizi mbovu katika mtandao wenu?Haiwezekani kwamba gazeti kubwa kama Daily News litakosa angalau shabiki mmoja wa CHADEMA na mgombea wake, na pia lazima wamo wanachama wa CHADEMA katika gazeti hilo. Mmoja wao anaweza kuwa alipenyeza taarifa hiyo bila mabosi wake kujua.
Ni kosa kubwa kuwalaumu waliosoma taarifa hiyo kwenye tovuti badala kuchukua hatua kwa hao wanachama/mashabiki wa CHADEMA ndani ya Daily News.
Mhariri wa Daily News anapenda sana kutumia neno tabloid bila kujua maana yake kamili. Inaelekea kwake tabloid ni gazeti lo lote ambalo si broadsheet, kwa maana ya gazeti lenye kurasa ndogo ndogo, tofauti na gazeti lenye kurasa pana.
Hajang’amua kwamba tafsiri hiyo ilikwisha kupitwa na wakati zamani, na kwamba si kila gazeti dogo ni tabloid, kwa sababu ndogo tu: magazeti mengi makini duniani siku hizi yanachapwa katika kurasa ndogo.
Ile picha iliyozoeleka miaka hamsini iliyopita ya Mwingereza ameketi katika bustani yake, mbele yake iko birika ya chai, mbwa wake pembeni, na mzee ameshika gazei lililomfunika uso mzima, imekufa; lakini mhariri wa Daily News hajui hilo kwa sababu kurasa pana 'bado zimemfunika'.
Mhariri huyu ananikumbusha zama za shule katika midahalo ya wanafunzi. Wakati ule tulikuwa tunapangana kati ya wale watakounga mkono hoja na wale watakaopinga. Unapokuwaunajenga hoja, kisha ukaangalia katika hadhara ya wasikilizaji na ukamwona fulani anaonekana anashabikia unayoyasema, unakuwa unasali ‘kimoyomoyo’ huyo bwana asije akasimama kukuunga mkono wakati wa michango ya wasikilizaji. Atakuharibia hoja yako kwa kusema mambo ambayo yataonyesha kwamba hoja nzima ni mbovu, huku yeye akidhani anakusaidia kujenga hoja.
Ndiyo ya mhariri wa Daily News. Bila shaka chama-tawala kinapenda mhariri huyo ashiriki kuisaidia kampeni ya chama hicho na ashambulie kila tabloid inayoshindwa kuona maajabu yaliyofanywa na serikali ya chama -tawala. Lakini hata watawala wetu wanaweza wakajiuliza kama kweli gazeti hilo linasaidia kujenga hoja, au linakuwa kama yule mchangiaji wa mdahalo tuliyekuwa tukimchelea shuleni!
Kwa mfano, tunaweza kujiuliza kama kweli watawala wetu wanapenda tuambiwe kwamba matokeo ya uchaguzi wa rais tayari yanajulikana na ukweli ni kwamba Slaa hatakuwa rais? Watawala wetu wanajua hilo, na kama wanajua, wamelijua kwa njia ipi?
Naelewa vyema kwamba uchaguzi wetu umetawaliwa sana na kila aina ya ushirikina, na kwamba wanajimu na mafundi wa makafara wana nafasi muhimu katika kutuamulia ni nani anafaa kuwa kiongozi.
Hata hivyo, inaelekea mganga anayetumiwa na mhariri wa Daily News ni mkali kweli kweli kwa sababu amekwisha kutabiri kwamba Slaa hatakuwa rais siyo tu mwaka huu lakini hata miaka mitano baadaye.
Anasema mhariri huyu anayetufundisha maadili ya uandishi:And the truth of the matter is that Dr. Willibrod Slaa will not be the fifth president of Tanzania.Halafu mhariri anakusanya ujasiri wa ajabu kwa kusema kwamba Slaa ana matatizo ya kifamilia ambayo anatakiwa atumie umahiri wa kiuongozi kuyatatua. Nasema kwamba huu ni ujasiri wa ajabu kwa sababu, bila hata kuwadodosa wenzangu, inahitaji ujasiri kwa mhariri huyo kutamka hilo.
Tunasimuliwa na Biblia kwamba Bwana Yesu aliwakuta Wayahudi wamechachamaa, wameamua kumuua mwanamke mzinzi kwa kumpiga mawe, kama ilivyokuwa ifanyike nchini Iran majuzi. Bwana Yesu akasema: Yule ambaye hajawahi kutenda kosa kama hili, na awe wa kwanza kurusha jiwe. Walitawanyika wote!
Mhariri wa Daily News, kama angalikuwapo, angerusha jiwe?
Pages
▼
No comments:
Post a Comment