Wanamtandao wampa Dk. Slaa ushindi 76%
Daily News walimkubali kwa 60%Synovate wakana madai ya CHADEMA kumpa 45%WAKATI kampuni ya kibiashara inayojihusisha na tafiti ya Synovate Limited ikikanusha taarifa za kubaini kwamba mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa sasa anakubalika zaidi, Watanzania wanaotumia mitandao wamempa mwanasiasa huyo asilimia kubwa ya ushindi kulinganisha na wagombea wengine.
Ufuatiliaji wa Raia Mwema, katika mitandao mbalimbali ukiwamo ule wa gazeti la Serikali la Daily News (Daily News Online Edition) na mtandao maarufu kwa mijadala wa Jamiiforums unaonyesha kwamba Dk. Slaa anakubalika zaidi katika mtandao kuliko wagombea wengine akiwamo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, kumekuwa na angalizo katika mitandao kwamba si Watanzania wengi wanaotumia mitandao hata kama kuna ongezeko kubwa la matumizi ya mtandao kupitia simu za mikononi, hoja ambayo bado inaweza kutoa taswira tofauti katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, kutokana na wapiga kura wengi kuishi vijijini na wanaoishi mijini kutofahamu chochote kuhusu mtandao kama anavyosema na mchangiaji mmoja katika mtandao wa Jamiiforums:
“Ingekuwa JF (Jamiiforums) inasomwa na asimilia 50% tu ya Watanzania wote, basi, Dk. Slaa angepita kiurahisi sana. Lakini kwa kuwa wengi hawapiti humu inabidi juhudi za ziada zifanyike kushinda”.
Kura za maoni zilizokuwa zikiendeshwa na Daily News zikiwa na swali: ‘Will Dr. Slaa win the presidential race? ‘ (Je, Dk. Slaa atashinda urais?) zilionyesha kwamba kati ya watu 161 wa mwanzo waliopiga kura walionyesha kumpa Dk. Slaa asilimia 60.87 na ‘Hapana’ walikuwa asilimia 28.57, kabla ya kura hizo kusitishwa, kutokana na taarifa za kuwapo hofu ya ‘uchakachuaji’ uliodaiwa kufanywa na wafuasi au wapinzani wa Dk. Slaa.
Kwa upande wa mtandao wa Jamiiforums, zaidi ya watu 6,420 wamepiga kura hizo za maoni na kuonyesha kwamba Dk. Slaa amekubalika kwa watu 4, 895 sawa na asilimia 76.25 akifuatiwa na Kikwete ambaye anaonekana kukubalika kwa watu 779 katika mtandao huo, sawa na asilimia 12.13 akifuatiwa kwa karibu zaidi na Hashim Rungwe wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 448 (6.98%) wakati mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akikubalika kwa watu 205 (3.19%) na Mutamwega Mugahywa wa TLP akikubalika kwa watu 93 (1.45%).
Mwazilishi wa mada hiyo ya kura za maoni aliweka swali “Je,Mtanzania gani anafaa kuwa Rais wetu 2010?” Kabla hata ya majina ya wagombea kutangazwa na yeye mwenyewe kutangaza kuwania nafasi hiyo, Dk. Slaa alikuwa akitajwa kuwania nafasi hiyo na orodha ya majina kubandikwa mtandaoni badaa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza orodha ya wagombea hao.
Wachangiaji wengi katika mtandao huo wa Jamiiforums ambao baadhi ya watu wanautuhumu kupendelea wapinzani, wamekuwa wakitoa sifa kuu za mtu anayestahili kuwa Rais wa Tanzania na kumchambua Kikwete kuwa amepoteza sifa za kuendelea na nafasi hiyo kutokana na kushindwa kupambana na ufisadi kikamilifu kama alivyoahidi wakati akiingia madarakani mwaka 2005.
Miongoni mwa sifa walizoanisha katika mtandao huo ni pamoja na kuwa Rais ajaye anatakiwa awe ni msomi, mkimya, mchapa kazi, hana makundi na asiye na chembe ya ufisadi.
Kabla ya majina ya wagombea kutangazwa, wachangiaji waliwataka wagombea wa Upinzani mwaka 2000 na 2005 wasijitokeze tena mwaka huu akiwamo Freeman Mbowe wa CHADEMA, Lipumba wa CUF, Augutine Mrema wa TLP na John Cheyo wa UDP kwa maelezo kwamba matokeo ya nyuma yanaonyesha kwamba hawana jipya mwaka huu.
“Wanachotakiwa kukifanya sasa hivi ni kumchagua mtu tofauti kabisa. CCM hawawezi kubadilika. Rais ni nafasi ya Slaa sasa kwa ajili ya kusafisha na kuziba mianya ya ufisadi mkubwa. Baada ya hapo tunaweza kuchagua Rais mchumi ili ajenge uchumi wa nchi. Kwa sasa lazima tuondoe ufisadi kwanza, CCM hawawezi kuuondoa.
“Kikwete alisema anawajua wala rushwa, wauza madawa ya kulevya, wezi wa EPA waliorudisha fedha na wale wahujumu wa Bandarini lakini kashindwa kuwataja wala kuchukua hatua ilhali yeye tumempa mamlaka yote kikatiba ili ailinde nchi hii na mali zake.
“Slaa ni mzalendo wa kweli maana pamoja na kuwa hana mamlaka ya kuwafanya lolote mafisadi lakini kawataja hadharani bila woga au kuumauma maneno ingawa anajua hatari inayomkabili kupambana na watu wa aina hiyo. Huyu akipewa mamlaka ya kuongoza nchi mafisadi, wezi wa mali za umma nk, itabidi wakajichimbie makaburi wajizike wenyewe. Slaa ndio Rais anayefaa kwa wakati huu tulionao,” anasema mchangiaji mmoja wa Jamiiforums.
Baadhi ya vyombo vya habari wiki hii vilimnukuu Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akisema kuwa CHADEMA ina matokeo ya kura za maoni za Synovate yanayoonyesha kuwa Dk. Slaa anakubalika kwa asilimia 45 akifuatiwa na Rais Kikwete mwenye asilimia 41, kauli iliyowalazimu Synovate kukanusha.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Jumatatu, Meneja wa Synovate Limited, Aggrey Oriwo alisema taarifa hizo ni za kughushi, hazina ukweli wowote na zinaupotosha umma kwa kuwa hawajawahi kufanya utafiti wowote unaohusu kukubalika kwa wagombea wa urais.
Oriwo alisema kwa kawaida kampuni yao hufanya utafiti wa hali ya kisiasa kila baada ya miezi mitatu na kwamba wanatarajia kufanya hivyo kabla ya Oktoba 31 na kutoa taarifa yao, kauli iliyotolewa pia na Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu Demokrasia Tanzania (Redet), ambao nao wanatarajia kufanya utafiti wa mgombea anayekubalika.
2 comments:
TATIZO HAPA NI KUWA USALAMA WA TAIFA HAURUHUSU MPINZANI KUWA JUU YA RAISI HII INATOKANA NA KWAMBA BADO NI RAISI. DAILY NEWS WAO WAMEKWISHA TOA MAJIBU YA UCHAGUZI KWAMBA DR SLAA HATAKUWA RAISI WA TANO IKIWA NA MAANA KUWA HATA KAMA AKISHINDA HATAKABIDHIWA MADARAKA! HII NI DEMOKRASIA ISIYOZINGATIA MATAKWA YA WAPIGA KURA.
Mi nadhani huo ni msimamo wa serikali, na ndo maana hutujasikia na hatutasikia chombo chochote kikimkemea si mhariri wa gazeti, kwani Daily News ni mdomo wa serikali.
Kumlaumu Mkumbwa au gazeti tutakuwa tunakosea, kwani huyu ni mhariri makini anajua kile anachokiandika na maana yake, yawezekana kabisa kuwa ule ni msimamo wa serikali na imetumia kinywa chake kuwasilisha kwa wananchi.
Post a Comment