Pages

May 5, 2010

Kikongwe apinga hotuba ya JK.

WAZEE zaidi ya 1,000 waliokuwa wakimsikiliza Rais Jakaya Kikwete juzi kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee walikuwa wakimshangilia mara kwa mara, lakini si Bi Asha Omary, 70, aliyekuwa kijijini kwake wilayani Kisarawe.

Kikongwe huyo alisikiliza hotuba hiyo, iliyobatilisha mgomo wa wafanyakazi uliopangwa kuanza leo, kwenye redio akiwa Kijiji cha Bwana, Kata ya Kibuta na hasira alizopata kutokana na kauli za rais, zilimfanya aamue kusafiri takriban kilomita 35 kuanzia saa 1:00 asubuhi kuja jijini Dar es salaam kueleza jinsi alivyokerwa.

“Kama kiongozi wa taifa, rais angetumia maneno ya busara na hekima yasiyo na ukali ndani yake katika kutatua tatizo kwa sababu wafanyakazi wanadai haki yao na wanayo haki ya kufanya hivyo,” alisema Asha alipofika ofisi za gazeti la Mwananchi majira ya saa 4:30 jana.

“Rais amejisahau na anatumia vibaya mamlaka aliyopewa na Watanzania kuwakandamiza wafanyakazi, amesahau kuwa nafasi hiyo imetokana na wananchi wote wakiwapo hao wafanyakazi.”

Bi Asha alikuwa akizungumzia hotuba ya Rais Kikwete kuhusu mgomo wa wafanyakazi uliopangwa kuanza leo, hotuba ambayo iliwashambulia viongozi wa Tucta kuwa ni "waongo, wanafiki, wazandiki na wafitini" kwa madai kuwa wamekuwa hawawaelezi wanachama wao kuhusu maendeleo ya mazungumzo baina ya pande hizo.

Katika hotuba hiyo ya dakika 95, ambayo pia ilirushwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), TBC Taifa na redio Uhuru, Rais Kikwete, ambaye alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na wazee hao ambao wengi walivalia mavazi ya rangi za njano na kijani, alitangaza mgomo huo kuwa ni batili kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.

Bi Asha, ambaye ni mkulima wa jembe la mkono, alisema rais hakutumia hekima na busara katika kutatua kero za wafanyakazi bali alitumia cheo chake kuwatisha wafanyakazi katika kutetea haki zao.

Alisema kwamba serikali inapaswa kuweka umuhimu wa kutatua kero za wafanyakazi kwa kuwa ndio wanaotoa huduma zote muhimu kwa wananchi wote hasa masikini ambao ni wakulima.

Alisema rais na familia yake wanatibiwa nje ya nchi ndiyo mana haoni umuhimu wa kutatua kero za wafanyakazi badala yake anatoa majibu ya dharau kuwa kama hawataki kufanya kazi waache.

“Au kwa kuwa rais na viongozi wenzake wanatibiwa Ulaya na Marekani ndio maana anatoa vitisho au anataka uwe kama mgomo wa mwaka juzi kwenye Hospitali (ya Taifa) ya Muhimbili ambako watu walipoteza maisha,” alihoji Asha.

“Kama wafanyakazi nao wakisema liwalo na liwe wakachukua hasira kama alizochukuwa rais, itakuwaje; madaktari, manesi na watumishi wengine wakigoma, je haitasababisha maafa kwa Watanzania?”

Asha ambaye alitumia muda wa dakika 70 kueleza masikitiko yake, alisema wakati rais anawatisha wafanyakazi ili wasigome, anapaswa kufunga safari kwenda maeneo ya vjijini kujionea hiyo misaada ya matrekta na ‘Power Tiller’ kama imewafikia wananchi au inatumiwa na viongozi wa vijiji kwa maslahi yao.

Rais katika hotuba yake alisema serikali haiwezi kulipa kima cha chini cha Sh315,000 kwa watumishi wa umma kwa sababu wananchi wengine watakosa huduma za afya, pembejeo za kilimo na hata vifaa vya elimu na walimu.

“Sisi wakulima hatuwezi kugoma lakini kwa muda mrefu hata hizo pembejeo na matrekta anayoyazungumzia hatuyaoni, mbona hachukui hatua na kutoa hotuba kali kwa maafisa wake ili na sisi tupate hizo pembejeo,” alihoji Asha ambaye ni mtoto pekee katika familia yao.

“Sisi vijijini hatuna huduma bora za afya, maji, barabara, shule na rais anasikia kila siku Watanzania wakilalamikia hali hiyo. Je kwa nini rais asitumie cheo chake kuchukua hatua kutatua matatizo ya wananchi kama alivyoamua kwa wafanyakazi,” alisema Asha kwa hasira.

Akizungumzia kupanda kwa gharama za maisha, Asha alisema enzi za utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, bei za vyakula zilikuwa zinafanana katika maduka yote, lakini sasa kila mfanyabiashara ana bei zake.

“Je serikali inashindwa kusimamia tatizo la kupanda kwa gharama za maisha au rais anawaogopa wafanyabiashara... na kama anawaogopa itakuwaje kwa Watanzania,” alihoji Asha.“Namuomba rais siku moja angalau afanye ziara ya kupita katika maduka na kuhoji au kuangalia bei za vyakula halafu alinganishe na vipato vyetu sisi Watanzania kama tunamudu.”

Katika harakati za kutatua tatizo la ugumu wa maisha yake, bibi huyo alisema alishaenda ikulu mara mbili na kugonga hodi ofisi ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), inayoongozwa na mke wa rais, Mama Salma Kikwete ili kuomba mkopo kwa ajili ya kufanya biashara.Asha alisimulia kuwa alifanikiwa kuonana na mmoja wa watendaji wa Wama na kumuelea shida yake, lakini alijibiwa kwamba fedha za Wama zina mlolongo mrefu na kwamba yeye hawezi kuzipata.

“Nilipohoji ni mlolongo gani, hakunifafanulia ila aliishia kuniambia tu kwamba ni mkubwa na huwezi kupata fedha hizi... rudi nyumbani. Nikamuuliza je hizo fedha mnazotangaza kwamba mnawakopesha wanawake ni wanawake wote au mna wanawake maalum ambao wanastahiki, sikupata jibu,” alisema Asha huku akionekana kuwa na hasira.

Baada ya hapo nilijua kuwa fedha za Wama ni za watu maalum na sio kila mwanamke.

Hata hivyo, Asha alimuomba Mwenyezi Mungu ampe amuweke katika afya njema Rais Kikwete ili aweze kutumia hekima na busara katika uongozi wake; amuepushe na kutumia ubabe na cheo chake katika kuwaongoza Watanzania.

“Uongozi ni dhamana aliyopewa na Mwenyezi Mungu na Mwenyezi: Mungu pia ndiye anayeweza kumnyang’anya dhamana hiyo wala si Watanzania kama anavyodhani, hivyo ajitahidi kuwa mwadilifu, mwenye hekima, busara na imani katika uongozi wake,” alisema Asha.Pia aliwaombea wafanyakazi ambao wanataka kuingia katika mgomo kutofanya hivyo kwa kuwa wakifanya hivyo watadhulumu haki za Watanzania.

“Nawaombea kwa Mungu viongozi wa Tucta wawashawishi wafanyakazi wasigome ili wasibebe dhima ya kudhulumu haki za Watanzania watakaokosa huduma mbalimbali kwa muda wote watakaogoma, Aaaammmiiin,” alisema Asha ambaye ni mkulima wa kilimo cha jembe la mkono.

source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment