MALUIMBANO kuhusu waraka wa Kanisa Katoliki (RC) yanaendelea kuwa makali, baada ya waumini wa kanisa hilo kumuelezea mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru kuwa amepwelea.
Mbali na kauli hiyo iliyotolewa jana na Baraza la Walei, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Valentino Mokiwa amemtaka Kingunge kuliomba radhi kanisa badala ya kuombwa radhi kama alivyotaka.
Matamko hayo mazito yalitolewa kwa nyakati tofauti jana wakati wahusika hao walipokuwa wakizungumza na gazeti hili kuhusu utashi wa Kingunge kuwa Kanisa Katoliki limuombe radhi na kuungama kutokana na kumwita kuwa ni mkongwe.
Mwenyekiti wa Baraza la Walei, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Balozi Nicholas Kuhanga alisema baraza limewataka maaskofu wa kanisa hilo, kutoendelea kujibishana na Kingunge badala yake kazi hiyo sasa itafanywa na baraza hilo. Kuhanga, ambaye amewahi kuwa waziri, alisema wamefikia uamuzi huo kwa kuwa baraza linamjua kwa undani mwanasiasa huyo kwa kuwa wanaishi naye.
Balozi Kuhanga alisema anamshangaa Kingunge kuupinga waraka huo wakati unawasisitizia wananchi kuwachagua viongozi waadilifu na wanaojali maslahi ya wananchi. Alisema kanisa haliwezi kumwomba radhi Kingunge kwa kuwa hana tofauti na mafisadi kutokana na kitendo chake cha kupinga waraka unaowapinga mafisadi.
"Yeye anaingia katika kundi hilo, (Mafisadi) kutokana na msimamo wake wa kuupinga waraka huo unaopinga ufisadi nchini," alisema Kuhanga. "Wale ambao hawana hulka za kifisadi wanaunga mkono waraka wakati wale ambao wana hulka za kifisadi wanaupinga, kwa sababu unatishia maslahi yao." Alifafanua kuwa waraka huo umetolewa kama somo la uraia ambalo limeonekana kufifia na kusababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii.
source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment