Pages

August 19, 2009

ASKOFU MAYALA AFARIKI DUNIA

Habari zilizotufikia kutoka Rock City zinasema kuwa Askofu Mkuu Anthony Mayala( 69) wa Kanisa Katoliki Mwanza amefariki dunia leo mchana katika Hospitali ya Bugando alikopokelewa baada ya kuugua ghafla.
Taarifa kutoka Mwanza kwa Msaidizi wake, Padri Renatus Nkwande zilieleza kuwa Askofu Mkuu Mayala aliugua ghafla saa mbili asubuhi baada ya kuishiwa nguvu na alikimbizwa katika hospitali hiyo kabla mauti hayajamkuta saa 8:30 mchana.
“Hatutajua ni nini zaidi maana alikuwa mzima na asubuhi ali-collapse ghafla tukamkimbiza hospitali,” alisema Padri Nkwande ambaye alifafanua kuwa awali Askofu Mayala alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo mara kwa mara.
Alisema Jimbo hilo limepokea kwa masikitiko taarifa za madaktari kuhusu kifo hicho na kuongeza kuwa Jimbo limempoteza msimamizi aliyekuwa wakati wote msikivu wa shida za watu bila kujali imani zao, mcha Mungu, mpole na mnyenyekevu wa kuigwa na kwamba daima hakupenda kupigizana kelele na watu hata kama nafasi yake ingemruhusu kufanya hivyo.
Alisema utaratibu wa mazishi utafanywa na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) kwa kushirikiana na Jimbo hilo na kwamba taarifa zaidi zitapatikana kesho.Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TEC, Anthony Makunde alithibitisha taarifa za kifo cha Askofu Mayala na kueleza kuwa taarifa nyingine za maziko ya Askofu Mayala zitaelezwa baadaye.Askofu Mkuu Mayala alipata daraja la Upadri mwaka 1970 na mwaka 1979 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Musoma kabla ya kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza mwaka 1988.
Sisi tunasema Bwana Alitoa na Bwana ametwaa Jina la Bwana lihimidiwe.

1 comment: