Pages

January 30, 2009

Kilio cha Mtu mzima.......

Ukiona mtu mzima analia basi ujue kuna makubwa yamemkuta, hapana shaka aliyokutana nayo au kuyasikia toka kwa waathirika wenyewe yaani Maalbino maalufu kama "kinywa cha farasi" alishindwa kuzuia chozi lake akifafanua kwa waheshimiwa hasa waliomshutuma kuwa alikuwa ameenda kinyume na katiba.

Akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed, ambaye ni Mbunge wa Wawi (CUF), kwa uchungu, Pinda alisema kauli aliyoitumia ni katika kuwahakikishia wauaji hao kuwa Serikali sasa imechoshwa na unyama wanaoufanya na wasidhani Taifa na Watanzania watawavumilia.

“Pengine kuna mtu ambaye hajapata nafasi ya kuonana ana kwa ana na kuzungumza na watu hawa (albino), mimi nimekutana nao nimeona jinsi wanavyoumia (analia), mimi nilisema kuwa wauaji hawa hawawezi kuvumiliwa,” alisema Waziri Mkuu huyo na kukatisha kidogo hotuba yake na kulia.

Huku akifuta machozi, aliendelea kusema iwapo kuna Mtanzania ambaye anaona kuwa ametenda uovu kuliko maovu yote katika suala hilo la albino na iwe hivyo, lakini nia yake ilikuwa nzuri. Alisema alianza ziara yake katika Mkoa wa Tabora, baada ya kupewa kiundani historia ya mauaji hayo ambayo yalianzia kwa vikongwe ambao kwa takwimu alizopewa, waliouawa kwa mapanga walifikia 2,000 kwa sababu za kishirikina.

Alisema wakati mauaji hayo yakiendelea kukemewa, mwaka 2006 yalianza mauaji ya albino kwa kasi ndogo, lakini hadi juzi akiwa katika ziara hiyo, alipewa takwimu kuwa walifikia 28 na wengine watatu wakauawa akiwa bado katika ziara hiyo.

Aliongeza kuwa kwa watu ambao wameyashuhudia mauaji hayo, si mazuri na ni ya kutisha kwa kuwa wauaji wanachotaka ni viungo. “Tukio la Januari 22 wenyewe mliona yule baba wa watu alipokatwa mguu wa kulia na kisha kutelekezwa hapo, damu ilimwagika hadi akafa.” Alisema pamoja na Tanzania kusifika ndani na nje ya nchi kuwa ni nchi yenye amani na utulivu, mauaji hayo sasa yameitia doa nchi.

“Kutokana na mazingira haya, niliamua kufanya ziara na katika ziara yangu nilisisitiza umuhimu wa vyombo vya Dola katika kudhibiti mauaji haya, elimu kusambazwa kwa wananchi, kuongezwa kwa huduma za afya, madhehebu ya dini kukemea mauaji hayo na vyama vya siasa kuungana katika kupambana na tatizo hilo,” alisema.

No comments:

Post a Comment