Pages

January 30, 2009

AJARI ZAZIDI KUTUMALIZA BONGO.

Leo hii alfajili.
WATU 15 wamefariki dunia kutokana na ajali ya magari na gari moshi zilizotokea alfajiri ya kuamkia jana katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro, huku zikiacha majeruhi zaidi ya 20.
Mkoani Dar es Salaam, watu tisa walikufa papo hapo na wengine 10 kujeruhiwa katika eneo la Jet Club Kipawa katika Barabara ya Nyerere wakati mkoani Morogoro, watu sita wamekufa papo hapo na wengine 10 kujeruhiwa katika ajali ya gari moshi mali ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) iliyotokea katika maeneo ya Stesheni ya Mzaganza na Kidete katika Wilaya ya Kilosa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema ajali ya Kipawa ilitokea saa 10 alfajiri ambako gari lenye namba za usajili T700 AFT aina ya Toyota Hiace ‘Kipanya’ lililokuwa likitokea Airport kwenda Tazara, liligonga gari lenye namba za usajili T452 ACP aina ya Scania lililokuwa limeanguka katikati ya barabara na kusababisha kifo cha abiria tisa papo hapo.
Aliwataja baadhi ya waliokufa kuwa ni Ally Issa (37); Michael Maujiro; Augustino Yohana; Elly Athumani; Alfonsi Golesh; Machel Msagira (33); na John Steven.
Alisema maiti zote zimehifadhiwa katika Hospitali ya Amana wakati majeruhi 10 wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Alisema chanzo cha ajali hiyo, Kova alisema ni mwendo kasi wa dereva wa Hiace ambayo ilikuwa imebeba abiria ikitokea Machinjioni Pugu. Alidai imebainika gari hilo lilikuwa linafanya kazi usiku tu kutokana na muda wa leseni yake kumalizika.
Naye Ofisa Habari Msaidizi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Mary Ochieng, alisema hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri kiasi.
“Tunaendelea kuwapa matibabu…mmoja bado yupo ICU (chumba cha uangalizi maalumu) na tayari tumeshawaruhusu wawili,” alisema Ochieng jana mchana.
Waliolazwa ni Simon Silvesta (27); Eva Joseph (28); Karunde Osambi (32); Zamoyoni Mongera (36); Joshua Jumanne (29), Alex Msuya (65); Emilly Steven (40); Ratibu Abdallah (21).
Katika ajali ya Morogoro, ilitokea saa saba usiku wa kuamkia jana ikihusisha gari moshi lenye namba 8828 likiendeshwa na Richard Mkude (38) kwa kushirikiana na Msaidizi wake Lucas Isaya, wote ni wakazi wa Mkoa wa Morogoro.
Gari moshi hiyo iliyokuwa na mabehewa manne, ilikuwa ikitokea mikoa ya Bara kwenda Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Reli, Yessaya Msigwa, alithibitisha ajali hiyo na akizungumza kwa simu akiwa eneo la tukio, alisema katika mabehewa hayo manne, moja lilikuwa la abiria, jingine lilikuwa tupu wakati jingine lilibeba mataluma yakitokea Wilaya ya Mpanda mkoani Rukwa.
Alisema gari moshi hilo lilipofika Kijiji cha Msaganza, behewa la moja la nyuma liliyumba na kufuatia behewa lililowabeba abiria na baadaye yote kupinduka na kusababisha vifo vya watu hao na majeruhi hao walikuwa wakitoka mnadani.
Kamanda Msigwa aliwataja waliokufa katika ajali hiyo ni wafanyabiashara Said Pindupindu, Seif Bakari, Nassoro Mohamed, Jonas Lukanda, Abbas Kandaro; wote kutoka Wilaya ya Kilosa na mwingine mmoja ambaye jina lake halijatambuliwa.
Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa ni Hamisi Chamwitu; Seleman Mohamed, Sadic Monera, Esta Mbwambo na Asha Hamis ambao ni wakazi wa Mkoa wa Morogoro.
Wengine waliolazwa katika hospitali hiyo ni Edward Athanas, Aziz Seleman ambao ni wakazi wa Dar es Salaam; Hamis Manyeleta, Hamis Selemani, Mecha Jackson ambao ni wakazi wa Wilaya ya Kilosa.
Kamanda huyo alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
Alisema kazi ya kutambua miili hiyo ikikuwa ikiendelea na hadi kufikia jana mchana, miili ya watu watano kati ya sita ilikuwa imeshatambuliwa na ndugu zao na majeruhi wanaendelea vizuri.

1 comment:

  1. Kaka, jumamosi iliyopita niliandika TUMECHOSHWA NA SALAMU ZA RAMBIRAMBI NA SASA HATUZITAKI ( http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/01/tumechoshwa-na-salamu-za-rambirambi-na.html ) na kwa kutumia picha zako na za Kaka Michuzi nilieleza yale ambayo yametuchosha. Sasa sikia chanzo cha ajali hiyo. Mwenye gari atafanywa nini? Nasubiri kuona kama kuna atakayelipwa na bima ama pesa itakayotokana na kufilisiwa kwa mali za mwenye gari hiyo. Hakuna namna ya kumlipa aliyepoteza maisha yake, lakini pia hakuna namna ya kuendeleza yatokeayo.
    Poleni nyote

    ReplyDelete