Pages
▼
August 17, 2008
Brig General Nyambibo atunaye tena
JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA
Agosti16, 2008
PRESS RELEASE
Mkuu wa Chuo cha Kijeshi (TMA), Monduli Arusha, Brigedia Jenerali January Nyambibo amefariki Dunia katika Hospitali Kuu ya Kijeshi Lugalo Agosti 15, 2008 kwa ugonjwa.
Mipango ya mazishi inafanywa na Makao Makuu ya Jeshi kwa kushirikiana na familia yake. Msiba uko nyumbani kwa kaka yake Luteni Kanali Mstaafu Jackton Nyambibo, Gongo la Mboto Ukonga jijini Dar es Salaam karibu na hospitali ya Mather Care.
Marehemu atazikwa kwa heshima zote za kijeshi Jumatatu, Agosti 18, 2008 saa kumi alasiri katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Wakati wa uhai wake, Brigedia Jenerali Nyambibo alishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo, Msaidizi wa Mnadhimu Mkuu, Mkufunzi Mkuu TMA na Shule ya Mafunzo ya Infantria (SMI) Mgulani, Mwambata Jeshi nchini Msumbiji na Mkuu wa Chuo TMA wadhifa aliokuwa nao hadi alipofariki dunia.
Marehemu Nyambibo alizaliwa mkoani Mara mwaka 1953 na kupata elimu yake ya msingi na Sekondari mkoani Mara hadi mwaka 1971 alipojiunga na Jeshi la ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wakati wa utumishi wake jeshini, marehemu alipandishwa vyeo katika ngazi mbalimbali na kupata cheo cha Brigedia Jenerali Agosti 30, 2006 cheo alichofariki nacho.
Brigedia Jenerali Nyambibo atakumbukwa kwa mchango wake alioutoa wakati wa ukombozi Kusini mwa Afrika pale alipokuwa Kamanda wa Kikosi Maalum cha Mgagao mkoani Iringa kilichokuwa na jukumu la kuwafundisha wapigania uhuru wa Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini.
Imetolewa na Kitengo cha Habari
Makao Makuu ya Jeshi
Upanga, Dar es Salaam
RIP.
No comments:
Post a Comment