Pages

November 9, 2011

Mbowe asakwa na Polisi, atakiwa ajisalimishe.


KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu pamoja na wanachama wengine 25 wa chama hicho wamekamatwa na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali.


Mbali na hao, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ametakiwa kujisalimisha mwenyewe polisi baada ya kutoweka katika Viwanja vya NMC Unga Limited baada ya polisi kufanya operesheni ya kushtukiza kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama hicho na viongozi wao waliokesha hapo usiku wa kuamkia jana.


Juzi, viongozi hao wa juu wa Chadema walitangaza kupiga kambi kwenye viwanja hivyo kwa siku tatu ikiwa ni shinikizo la kutaka mahakama itoe kibali maalumu cha kumtoa gerezani Kisongo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye naye anatuhumiwa kufanya mkusanyiko usio halali.


Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa alisema jana kwamba viongozi hao walikamatwa alfajiri ya kuamkia jana baada ya polisi kuvamia mkutano huo wa mkesha.


Mpwapwa alisema jeshi hilo lililazimika kuvamia na kuvunja mkutano huo baada ya chama hicho kukiuka masharti ya kibali cha mkutano kilichotolewa na polisi kilichowaruhusu kufanya mkutano wa hadhara uwanjani hapo kuanzia saa 8:00 mchana wa juzi hadi saa 12:00 jioni.


Alidai kuwa katika tukio hilo, Dk Slaa alikutwa na bastola aina ya Walther namba T2CAR 61074-327963 ikiwa na risasi saba huku mtu mwingine aliyemtaja kwa jina la Daniel Zedekia Ongong’o naye akikutwa na bastola aina ya Pietro Berreta namba H.447577 Cat 5802, ikiwa na risasi 10 ambazo alisema wanaendelea kuchunguza uhalali wa umiliki wake na sababu za wahusika kuwa nazo eneo hilo.


“Wakati Mheshimiwa Lissu alijisalimisha mwenyewe kwa polisi, Dk Slaa yeye tulimkamata akiwa ndani ya moja ya magari yaliyokutwa uwanjani hapo na hakukuwa na purukushani yoyote wakati wa kuwatia mbaroni watuhumiwa,” alisema Mpwapwa.


source: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment