Pages

October 19, 2011

JE WATAMANI AU KUTARAJI KUSIKIA NINI TOKA KWA LOWASSA?


WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa leo anatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari katika mkutano ambao utazungumzia mambo makuu matatu likiwamo suala la Kampuni ya kufua umeme ya Richmond ambalo lilisababisha ajiuzulu wadhifa huo, Februari 2007. 

Mkutano huo wa Lowassa unafanyika siku moja tangu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha, James Millya atoe matamshi makali akiwatuhumu aliowaita watoto wa vigogo kwamba wanavuruga umoja huo huku akilalamika kwamba: “Maisha yake yapo hatarini.” 

Habari zilizopatikana jana kupitia kwa watu walio karibu na Lowassa zinasema, katika mkutano huo, Mbunge huyo wa Monduli (CCM), pia atazungumzia taarifa zinazomhusu ambazo zimekuwa zikichapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini.

  Suala jingine ambalo linatarajiwa kuzungumzwa na kiongozi huyo ni kuhusu mgogoro ndani ya CCM mkoani Arusha, ambao unatokana na mgawanyiko miongoni mwa makada na viongozi wa chama hicho.  “Pia anasema kwamba ataanzia pale alipoishia, siku ile alipozungumza bungeni kuhusu Serikali kufanya uamuzi mgumu lakini hakutakuwa na kumshambulia mtu,” alisema mmoja wa watu hao na kuongeza:

  “Anasema (Lowassa) kwamba lazima aweke kumbukumbu sahihi kwa baadhi ya mambo ambayo yametamkwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na viongozi wengine kwani amebaini kuwa uongo ukisemwa sana na kwa muda mrefu hugeuka kuwa ukweli.”

Hii ni mara ya kwanza kwa Lowassa kuitisha mkutano wa vyombo vya habari tangu alipojiuzulu kuzungumzia sakata la Richmond ambalo halikuwahi kupata hitimisho la kisiasa wala kisheria.

Source: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment