Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla walipokea kwa
masikitiko, huzuni na majonzi makubwa taarifa ya kuzama kwa Meli ya MV.Spice
Islander katika Bahari ya Hindi karibu na Nungwi usiku wa kuamkia tarehe 10
Septemba 2011 ambapo watu 612 waliokolewa wakiwa hai na maiti 203 zimepatikana
mpaka sasa. Ili kujua ukweli kuhusu chanzo cha ajali hiyo, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar
imeamua kuunda Tume ya kuchunguza ajali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee inaeleza kwamba
kwa kutumia uwezo aliopewa chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi Sura ya 33 ya
Sheria za Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein ameunda Tume ya Kuchunguza Ajali ya
Kuzama kwa Meli ya MV. Spice Islander ambayo itakuwa na Mwenyekiti, Wajumbe na
Katibu kama ifuatavyo :-
- Mhe. Jaji Abdulhakim Ameir Issa – Mwenyekiti
- Meja Jenerali S.S Omari – Mjumbe
- COMDR. Hassan Mussa Mzee – Mjumbe
- Capt. Abdulla Yussuf Jumbe – Mjumbe
- Capt. Abdulla Juma Abdulla – Mjumbe
- Bw. Salum Toufiq Ali – Mjumbe
- Capt. Hatib Katandula – Mjumbe
- Bi. Mkakili Fauster Ngowi – Mjumbe
- Bw. Ali Omar Chengo – Mjumbe
- Bw. Shaaban Ramadhan Abdulla - Katibu
Mwenyekiti wa Tume hiyo , Mhe. Jaji Abdulhakim Ameir Issa ni
Mwanasheria mzoefu ambae kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Meja Jenerali S. S. Omari ni Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la
Wanamaji katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), COMDR. Hassan Mussa Mzee
ni Mkuu wa Kikosi cha KMKM na Capt. Abdulla Yussuf Jumbe ni Nahodha mzoefu wa
meli za kitaifa na meli za Kimataifa, ambapo pia aliwahi kuwa nahodha wa Meli
ya MV. Mapinduzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Capt. Abdulla Juma Abdulla, alikuwa katika Kikosi cha KMKM
kwa muda mrefu ambapo sasa ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Idara Maalum za SMZ na Bw. Salum Toufiq Ali ni Mwanasheria
wa siku nyingi Zanzibar ambae ana uzoefu wa sheria za bahari, ambae kwa sasa ni
Mwanasheria wa kampuni ya ZANTEL
.
Capt. Hatibu Katandula ni Mkufunzi katika chuo cha Ubaharia
cha Dar es Salaam na Bi Mkakili Fauster Ngowi ni
Wakili wa Serikali Mkuu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Tanzania.
Bw. Ali Omar Chengo aliwahi kuwa mwanajeshi katika JWTZ na
baadae kufanya kazi kwa muda mrefu katika Kikosi cha KMKM kabla ya kuwa Mjumbe
wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Naibu
waziri wa Mawasiliano katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huko nyuma.
Katibu wa Tume
hiyo Bw. Shaaban Ramadhan Abdulla ni mtaalamu wa Sheria za bahari, ambapo kwa
sasa ni Mwanasheria katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP).
No comments:
Post a Comment