Pages

September 20, 2011

Dr Kawambwa awakejeli walimu Nchini


SERIKALI imesema walimu nchini wangekuwa wanatumia nguvu kubwa wanayotumia hivi sasa kudai posho na malimbikizo yao, wangeitumia madarasani matokeo mabaya yangekuwa ni historia.

 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya uUfundi, Dk Shukuru Kawambwa, alisema hali ya ufundishaji madarasani hivi sasa hairidhishi kutokana na baadhi ya walimu wamekuwa hawatilii mkazo kanuni, taratibu na sheria ya maelekezo ya ajira zao. 

Alisema kutokana na hali hiyo, hivi sasa Serikali hairidhishwi na utendaji kazi wa baadhi ya walimu, kwani licha ya jitihada za kuhamasishana bado wanatumia nguvu kubwa kudai posho na malimbikizo mbalimbali na kwamba, wangetumia kasi hiyo madarasani matokeo mabaya yangekuwa ni historia. 

Dk Kawambwa, ambaye pia ni Mbunge wa Bagamoyo, alisema hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza Shule ya Msingi Milo huku akionyesha kutoridhishwa na hali aliyoshuhudia, kwani licha ya kuwapo wanafunzi 151, hakuna vitabu na miundombinu ni mibovu. 

Kitu kingine kilichomshangazwa, ni zaidi ya mwaka mmoja hakuna mahala panapoonyesha kuna maofisa wa elimu wa wilaya au wakaguzi waliowahi kutembelea shule hiyo hata mara moja.

 “Kwa kweli sijaridhishwa kabisa na hali hii niliyoikuta hapa, wanafunzi wapo 151 hawana vitabu, shule ina hali mbaya na zaidi kinachochefua hakuna kumbukumbu ya maofisa elimu au wakaguzi waliowahi kutembelea hapa hata mara moja,” alisema Dk Kawambwa na kuongeza: 

“Pia, nimepata picha halisi kuwa ni dhahiri kuna pengo kubwa la mawasiliano baina ya maofisa elimu, wakaguzi wa elimu na hata maofisa elimu wa mkoa siyo kwa Bagamoyo tu, inawezekana hali ni hii nchi nzima  kwa walimu wa shule za pembezoni mwa wilaya.”

 
Alikitaka Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kuongeza kasi ya kuhamasisha wanachama wake kutimiza wajibu wao, kwani kazi ya ualimu ni ngumu na inahitaji mtu ambaye ana wito wa pekee, hivi sasa wengi wao hawatimizi majukumu yao ipasavyo.

 Pia, kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Milo, Dk Kawambwa aliwataka kuwa na moyo wa kujitolea kujenga nyumba za walimu na kuahidi Serikali kuwaunga mkono, ili kupunguza tatizo la walimu kukaa mbali na vituo vya kazi.

Source Mwananchi

No comments:

Post a Comment