Pengine ni ndoto za mchana au ni jinamizi lilinikumba nikajikuta naota eti Mahakama ya Rufaa imeuzwa na ati inatarajiwa kuvunjwa, siamini, nadhani ni ndoto za mchana tu ndo zinanisumbua, sidhani kuwa serikali yangu hii, niloichagua na kuiweka madarakani inaweza kufanya jambo kama hilo, sidhani, na haiwezekani.
Ndoto za mchana uwa ni mbaya wakati mwingine, ni rahisi kuota umeokota bulungutu na kuamka ukiwa lofa zaidi, eti ile hoteli jirani yake imeihisi inabanwa na mahakama ile na sasa inataka iondoe kiwingu, ati wageni wakiona majoho ya waheshimiwa majaji wetu wanaweweseka vyumbani, mvinyo haupandi, wanaota majinamizi! Mhh ni kweli habari hii? Mbona yule kiongozi wa taifa kubwa kabisa duniani alilala hapo siku kadhaa na hakuweweseka? ahh, ndo mambo ya ndoto hayo unakurupuka unadhani ni kweli, walinganisha na uhalisia waona kuna walakini ndo wagundua, kumbe ni ndoto tu.
Lakini mbona ndoto hii imekuwa ndefu hivi? ati kuna wataalamu fulani (si wa sheria) wanataka kuandamana kupinga kuvunjwa kwa mahakama hii? mhh yawezekana bado niko ndotoni, hivi wanasheria si ndo wangekuwa wakwanza kuandamana? sasa iweje wale, wanaitwaje vileee?? enhee, wasanifu ndo wawe na kimbelembele kuandamana??? Si mwaona mambo ya ndoto hayo, lakini kama ingekuwa ni kweli hata mimi ningewaunga mkono, ningeandamana, sijui mpaka wapi, kokote kule.
Ahh! ndo mambo ya ndoto za mchana hayo, usiombe ukaota, zinadanganya sana, hebu we fikiria serikali makini kama hii kweli yaweza kufanya uamuzi wa kijinga kama huo? hata siku moja haiwezekani, ni ndoto hizo, tena za mchana, silali tena mchana nisije jikuta naota na Ikulu nayo imeuzwa bure!
Jamani puuzieni, ni ndoto tu.
Tanzania kila kitu kinawezekana, ukweli ama ndoto, vyote vinawezekana tu.
ReplyDelete