Pages

August 4, 2011

Kikombe cha Babu - 78% wamepona by Utafiti.


Juzi niliweka post hapa kujaribu kutafuta ushuhuda wa wale ambao walienda Loliondo Samunge kwa Babu kupata kikombe ili kujua kama kuna yeyote ambaye hakika kupitia kikombe amepata uponyaji, hakuna aliyejitokeza mpaka sasa. 
Leo hii Synovate wamekuja na utafiti unaoonyesha kuwa asilimia 78 wamepona. 



ASILIMIA 78 ya watu waliotibiwa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapila, walipona magonjwa yao.
Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Synovate kuanzia Mei 2 hadi 19, mwaka huu na kuwahoji watu 1,994 wenye umri zaidi ya miaka 18 maeneo mbalimbali nchini.Utafiti huo uliotolewa na Synovate kwa gazeti hili jana, unaeleza kuwa ni asilimia saba waliosema hawakupona wakati asilimia 15 walisema hawajui.
“Asilimia 78 ya waliotibiwa kwa kikombe cha Babu wa Loliondo, walisema wamepona magonjwa yaliyokuwa yanawakabili,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ya utafiti.
Utafiti wa Synovate umekuja wakati ambapo utafiti wa awali uliofanywa na serikali juu ya dawa hiyo ya Babu kuinyesha kuwa ina uwezo wa kutibu magonjwa sugu kama vile kisukari, saratani, moyo na Ukimwi.
Serikali ilisema bado inaendelea na utafiti zaidi juu ya dawa hiyo, ambao unaweza kuchukua muda wa hadi miaka mitatu ikizingatia kuwachunguza waliotibiwa na kiwango cha dozi, kulingana na aina ya ugonjwa.
Ripoti ya Synovate inaonyesha ingawa ni watu wengi wanaotamani kuponyeshwa dawa ya Babu, ni Watanzania wachache wenye uwezo wa kumudu gharama za kwenda Loliondo.

Asilimia 83 walisema ni vigumu kupata dawa ya mchungaji huyo maarufu kama Kikombe, huku asilimia 17 wakaonyesha hakuna tatizo la kumfikia.Hata hivyo, kati ya waliokwenda asilimia 25 hawakuwa tayari kutaja magonjwa waliyokwenda kutibiwa, wakati asilimia 24 walisema ni kisukari.
Magonjwa mengine na asilimia ya watu walioenda kutibiwa kwenye mabano ni moyo (22), Ukimwi (13), saratani (12), vidonda vya tumbo (7), pumu (5), magonjwa ya ngozi (4), maumivu ya miguu (4), kifua kikuu (3), maumivu ya tumbo (3), maumivu ya uti wa mgongo (2), maumivu ya kifua (2), macho (1) na waliokwenda bila tatizo maalumu (3).
Mchungaji Masapila alijijenga umaarufu mkubwa kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu baada ya watu kutoka sehemu mbalimbali nchini na nchi jirani kujitokeza kwa wingi kupata tiba hiyo.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya ndugu kuwachukuwa wagonjwa wao waliolazwa hospitalini kuelekea kwa Babu, yapata kilomita 400 kutoka mjini Arusha.

Misururu mirefu ya magari ilijipanga kwenda kwa babu na kufanya watu kutumia hadi siku saba kupanga foleni ya kupata dawa.
Pia, utafiti wa Synovate ulizingatia kuwa kulikuwa na waganga wa jadi waliojitokeza kutoa tiba sawa na Masapila, lakini licha ya hali hiyo, asilimia 60 walikiamini Kikombe cha Babu.
Wengine waliojitokeza na asilimia za kuaminika kwa watu kwenye mabano ni Dogo Jafferi wa Mbeya (9), Magret maarufu kama Bibi wa Tabora (8), Subira Ali (4), Majimarefu (2), Sinkala wa Mbuyuni (2) na babu wa Moma Mtwara (2). 


 source: Mwanachi
Picha: ©Emmanuel Herman

No comments:

Post a Comment