Pages

July 13, 2011

JAMANI TUMSAIDIENI KIJANA HUYU. ANATESEKA SANA


ABBAS Abdalaah (31) aliapoanza kuvimba uvimbe mdogo katika mguu wake wa kulia hakujua kuwa ulikuwa ni mwanzo wa ugonjwa ambao hatimaye ungemfanya ashindwe kutembea.Ugonjwa huo ambao mpaka sasa haujulikani, umemfanya Abbas kulala kitandni muda wote akilazimika kubebwa na watu watano kumpeleka nje kujisaidia.
 
Matumaini aliyokuwa nayo ya kupata tiba ya ugonjwa wake, yameanza kutoweka baada ya msamaria aliyejitokeza kumpeleka Hospitali ya Seliani mjini Arusha kushindwa kutimiza ahadi yake.
 
Abbas ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Kiru Ndogo, anasema vurugu za wananchi na wawekezaji wa Bonde la Kiru, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, ndizo anaona zimesababisha mpaka sasa asipate msaada.
 
“Vurugu hizi zilizoaanza Machi mwaka huu , ndizo zilizosabisha leo niwe bado hapa sina msaada, kwani mmoja wa wawekezaji katika Bonde hili alikuwa ameaahidi kunisaidia kunipeleka hospitali ya Seliani," anasema kwa uchungu akiwa amelala katika kitanda chake kilichopo sebuleni kwenye nyumba ndogo ya nyasi ya Bibi yake, Zuhura Abdalah.
 
Akisimulia historia ya ugonjwa wake huo, anasema alianza kuvimba kiumbe kidogo katika mguu wake mwaka 2005, wakati huo akiwa mchezaji mzuri wa mpira wa miguu kijiji hapo.
 
Anasema hakuwa na wasiwasi kwamba huo ungekuwa ugonjwa mkubwa ambao ungemfikisha hapo alipo.
 
Taratibu mguu ulianza kuvimba, hali ambayo ilimfanya baba yake mzazi, mzee Abdallah Juma  mwaka 2008, kumpeleka Hospitali ya Hydom, Wilaya ya Mbulu ambako baada ya kumchunguza hawakuona ugonjwa, ingawa mguu ulikuwa umevimba.
 
“Hydom hawakuona ugonjwa, nikawauliza mbona bado mguu umevimba kwa nini hamuoni tatizo, wakanishauri nirudi nyumbani, “ anasimulia kwa uchungu kijana huyu mchangamfu.
 
 Ingawa madaktari katika hospitali hiyo hawakuona tatizo lolote katika mguu wa Abbas, lakini mguu mzima ulizidi kuongezeka unene, mwaka 2009 wazazi wake wakaamua kumpeleka Hospitali ya Mission ya Dareda, Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
 
Huko waligundua alikuwa na matatizo katika seli za mwili hivyo wao hawakuwa na uwezo wa kumtibu na kumshauri aende Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo Moshi mjini mkoani Kilimanjaro.Anasema mwaka uliofuatia alikwenda KCMC ambako alifanyiwa uchunguzi na matokeo yalionyesha kwamba alikuwa na matatizo ya maji kujaa katika mguu na pia alikuwa na tatizo la nyama kuongezeka katika mguu wake.
 
Abbas anasema baada ya kungulika tatizo hilo aliuzwa na daktari wake kama ana uwezo wa kulipia matibabu ya ugonjwa wake nje ya nchi, lakini alisema hana uwezo.“Baada ya kueleza kuwa sina uwezo, basi huo ukawa ndio mwisho wa uwezo wao kunisaidia, nilirejea nyumbani nikiwa bado nina uwezo wa kutembea mwenyewe,” anasema.
 
Hata hivyo akiwa amekata tamaa ya kupata matibabu aliendelea kuishi huku akifanya shughuli zake za kila siku kwani mbali ya mguu kuendelea kuvimba , lakini hukuwa akisikia maumivu.Machi mwaka huu ndio mwezi ambao utabaki katika kumbukumbu zake zaidi kijana huyu, kwani ndipo aliposhindwa kutembea na kuwa mtu kulala kitandani.
 
Tangu wakati huu kasi ya mguu kuvimba iliongezeka huku akiwa hawezi hata kusimama kwani akitaka kutoka nje ya nyumba anatakiwa kubebwa na vijana watano wenye nguvu. Mbali ya kuvimba sasa ana kidonda ambacho kinamsumbua katika mguu huo.
 
 Wakati akiendelea kuwaza tiba ya ugonjwa wake, Mei mwaka huu mzazi wake alikwenda kumwomba mmoja wawekezaji katika Bonde lenye mgogoro la Kiru kumsaidia hela za matatibu katika Hospitali ya Selian Arusha, alikubali.Hata hivyo, kama waswahili wanavyosema ng’ombe wa masikini hazai , wakati akijindaa kumsaidia mgogoro mkubwa ukaibuka kati wa wananchi wenzake na wawekezaji  19 waliopo katika bonde hili, uliosabisha kuibuka vurugu.
 
Vurugu hizo zilizosababisha watu wawili kuuawa na mali za wawekezaji yakiwamo mashamba ya miwa na magari kuchomwa moto, zilifuta matumaini ya kupata msaada huo.“Naona huyu mwekezaji amekasirika kutokana na mgogoro au naye kakimbia makazi yake kutokana na vurugu hizi, sasa sina msaada mwingine,” anasema kwa masikitiko.
 
Anaomba mtu yeyote mwenye uwezo amsaidie kumpa hela za matibabu ili apone na kurejea katika hali yake ya kawaida.“Ninaomba watu wenye uwezo wanisaidie kunipatia hela niende hospitali  ili nami niwe kama watu wengine jamani, nateseka,” anasema.

 
Anayetaka kumsaidia awasiliane kwa namba 0786272409 au 0655304336



Bongo Pix inakupa pole sana Abas kwa maradhi hayo yanayokusumbua na tutatoa kamchango kidogo kulingana na uwezo wetu, pia tunakaribishwa wadau ambao watakuwa wameguswa kama sisi tulivyoguswa na wangependa kuchangia wanaweza kupitisha michango yao kwa 
M-PESA No 0764 927070 nasi tutaiwasilisha kwa muhusika mara moja au wawasiliane moja kwa moja kwa namba zilizotolewa hapo juu. Asanteni Sana.


Source: Mwananchi 

No comments:

Post a Comment