Majibu ya Zito kwa Bunge
NI VITA YA POSHO BUNGENI
Wabunge wa CCM na Chadema jana wakuwa na vikao vya ndani kwa ajili ya kuweka mikakati ya kujadili Bajeti Kuu ya Serikali, iliyowasilishwa bungeni Jumatano iliyopita. Mjadala wa bajeti unatarajiwa kuanza rasmi Jumatano ijayo.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni alisema posho zinazotakiwa kufutwa ni kwa watumishi wote wa umma ambao wamekuwa wakilipwa fedha za vikao hata wanapokuwa katika mazingira ya kutekeleza wajibu wao wa kila siku.
"Tumekokotoa na tunaendelea kukokotoa na inaelekea tunaweza kuokoa hadi kiasi cha Sh900 bilioni ikiwa posho zote zitafutwa, hili linawezekana kama tutakavyoonyesha katika bajeti yetu mbadala tutakayowasilisha Jumanne ijayo," alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema wabunge wamekuwa wakilipwa mishahara kwa mwezi pamoja na fedha za kujikimu (per diem) wanapokuwa nje ya majimbo yao kikazi na kwamba wanachopinga ni "posho za vikao" (sitting allowance) ambazo ni kikwazo cha utekelezaji wa kazi za Serikali na majukumu mengine katika ofisi za umma.
Alisema utoaji wa fedha za vikao uliasisiwa na Bunge na umesambaa taratibu katika taasisi nyingine za umma na kusababisha watendaji kutunga semina na vikao vingi alimradi wanapata posho huku kazi nyingine zikiendelea kulala.
"Kwa mfano, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Uongozi (ya Bunge), nasaini 'sitting allowance' katika kikao cha Bunge, nikiitwa katika kikao cha kamati ya uongozi nasaini tena sitting allowance na hata kama kutakuwa na kikao kingine jioni naweza kulipwa, sasa kama huo siyo wizi ni nini?"
"Huu ni wizi wa fedha za umma ambao umetaasisiwa na sasa unaathiri utendaji katika mfumo mzima wa serikali, si fedha tu kwani hata kazi zinalala kwani watendaji wote wanakimbilia kwenye vikao vya kutunga kwa sababu kuna posho na si vinginevyo."
Alisema hoja si malipo ya posho kwa wabunge wa Chadema pekee, bali kwa watumishi wa nchi nzima ambao ni zaidi ya 500,000 na kwamba malipo ya posho hizo yamesababisha kuwepo kwa tofauti kubwa ya kipato baina ya watu walioko kwenye menejimenti na watumishi wengine. |
No comments:
Post a Comment